Zaburi 63

Zaburi 63

Hamu ya kuwa pamoja na Mungu

1Ee Mungu, wewe u Mungu wangu,

nami nakutafuta kwa moyo;

roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu;

nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji.

2Nimetaka kukuona patakatifuni pako,

niione nguvu yako na utukufu wako.

3Fadhili zako ni bora kuliko maisha,[#63:3 Au, “Neema”; au, “upendo mkuu”. Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa linatumika mara kwa mara kuhusu vitendo vya Mungu kwa ajili ya watu wake ambao wana uhusiano naye kwa agano alilofanya nao.]

nami nitakusifu kwa mdomo wangu.

4Nitakushukuru maisha yangu yote;

nitainua mikono yangu na kukuomba.

5Roho yangu inafurahi kama kwa karamu na vinono;

kwa shangwe nitaimba sifa zako.

6Niwapo kitandani ninakukumbuka,

usiku kucha ninakufikiria;

7maana wewe umenisaidia daima.

Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

8Roho yangu inaambatana nawe kabisa,

mkono wako wa kulia wanitegemeza.

9Lakini hao wanaotaka kuyaangamiza maisha yangu,

watatumbukia chini kwenye makao ya wafu.

10Watauawa kwa upanga,

watakuwa chakula cha mbweha.

11Lakini mfalme atafurahi kwa sababu ya Mungu;

wanaoahidi kwa jina la Mungu watamsifu,

lakini vinywa vya waongo vitafumbwa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania