The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, watu wasiokujua wameivamia nchi yako.[#79:1 Neno “wasiokujua” linatumika hapa kutafsiria neno la Kiebrania “goyim”, yaani watu wasio Waisraeli au kwa maneno mengine “watu wa mataifa mengine”.]
Wamelitia najisi hekalu lako takatifu,
na kuufanya mji wa Yerusalemu kuwa magofu.
2Wameacha maiti za watumishi wako ziliwe na ndege,[#79:2 Maiti hizo hazikuzikwa kwa heshima kama ilivokuwa desturi ya Wayahudi na hivyo tukio hilo linaongezewa ubaya na aibu kwani miili iliyoachwa bila kuzikwa iliifanya hata nchi yote kuwa najisi.]
miili ya watu wako chakula cha wanyama wa porini.
3Damu yao imemwagwa kama maji mjini Yerusalemu,
wamelazwa humo na hakuna wa kuwazika.
4Tumekuwa aibu kwa mataifa ya jirani,
jirani zetu wanatucheka na kutudhihaki.
5Ee Mwenyezi-Mungu, je, utakasirika hata milele?
Hasira yako ya wivu itawaka kama moto hata lini?
6Uwamwagie watu wasiokujua hasira yako;
naam, tawala zote zisizoheshimu jina lako.
7Maana wamemmeza Yakobo, taifa lako,
wameteketeza kabisa makao yake.
8Usituadhibu kwa sababu ya makosa ya wazee wetu.
Huruma yako itujie haraka,
maana tumekandamizwa mno!
9Utusaidie, ee Mungu, mwokozi wetu;
kwa heshima ya jina lako
utuokoe na kutusamehe dhambi zetu,
kwa ajili ya jina lako.
10Kwa nini mataifa yatuambie:
“Yuko wapi Mungu wenu?”
Utujalie tuone ukiwalipiza watu wa mataifa
mauaji ya watumishi wako.
11Kilio cha hao wafungwa kikufikie;[#79:11 Baada ya kuteketezwa kwa mji wa Yerusalemu watu wengi walichukuliwa hadi Babuloni ambako walikaa bila matumaini ya kuweza kurudi tena makwao.]
kwa nguvu yako kuu uwaokoe waliohukumiwa kufa.
12Mataifa hayo yaliyokudharau, ee Bwana,
yalipizwe mara saba!
13Nasi watu wako, tulio kondoo wa kundi lako,[#79:13 Aya hii ya mwisho ni kama tamko la imani ya Waisraeli kwa Mungu na matumaini kwamba yeye ataendelea kuwajalia mahitaji yao kama mchungaji anavyochunga kondoo wake.]
tutakushukuru milele,
na kukusifu nyakati zote.