Zaburi 8

Zaburi 8

Utukufu wa Mungu na cheo cha binadamu

1Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wetu,[#8:1 Mwenyezi-Mungu: Kiebrania ni “Yahweh”, jina la Mungu wa pekee aliye mmoja tu. “Bwana” hapa, ni jina la sifa, nalo linatafsiri jina la sifa la Kiebrania “adon”. Tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) haitofautishi matumizi hayo mawili Yahweh/adonay ila inarudia neno lile lile: “kurie”, “ho kurios”, Kiswahili: “bwana”, “bwana”.]

kweli jina lako latukuka duniani kote!

Utukufu wako waenea mpaka juu ya mbingu!

2Kwa sifa za watoto wadogo na wanyonyao,

umejiwekea ngome dhidi ya adui zako,

uwakomeshe waasi na wapinzani wako.

3Nikiangalia mbingu, kazi ya vidole vyako,

mwezi na nyota ulizozisimika huko,

4mtu ni nini, ee Mungu, hata umfikirie,

binadamu ni nini hata umjali?

5Umemfanya awe karibu kama Mungu,[#8:5 Au, “umemwumba karibu awe kama wewe, ee Mungu”. Ukuu na fahari ya binadamu unadhihirika kwa vile alifanywa kuwa kidogo tu chini ya “elim” neno la Kiebrania ambalo maana yake kamili inatatanisha hapa na tunazo tafsiri mbalimbali: kidogo kuliko Mungu, kidogo kuliko malaika, (ndivyo katika tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta-LXX). Maana inayohusika hapa inaonekana wazi kutokana na aya 6-8 ambapo hali ya kutawala viumbe vyote ni hadhi yake Mungu mwenyewe lakini amemkabidhi binadamu (taz Mwa 1:26). Katika A.J. Zaburi hii imetumiwa kueleza hadhi yake Yesu mwenyewe ambaye ndiye mfano kamili wa Mungu (1Kor 15:27; Efe 1:22; Ebr 2:8).]

umemvika fahari na heshima.

6Ulimpa madaraka juu ya kazi zako zote;

uliviweka viumbe vyote chini ya mamlaka yake:

7kondoo, ng'ombe, na wanyama wa porini;

8ndege, samaki, na viumbe vyote vya baharini.

9Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wetu,[#8:9 Mwandishi au mtunzi anafunga Zaburi hii kwa kutumia maneno yaleyale aliyoanza nayo katika aya ya kwanza.]

kweli jina lako latukuka duniani kote!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania