Waroma 16

Waroma 16

Salamu kwa watu mbalimbali

1Napenda kumjulisha kwenu dada yetu Foibe ambaye ni mtumishi katika kanisa la Kenkrea.[#16:1 Kuhusu Foibe.; #16:1 Hapa si dada yao wa damu bali anaitwa hivyo kuonesha kuwa naye ni mmoja wao wanaomwamini Yesu Kristo. Walio waumini wanaume waliitwa ndugu na wanawake waliitwa dada, kwani wote wamekuwa tena watoto wa Mungu aliye Baba yao (ling Rom 8:15).; #16:1 Anatajwa hapa tu katika barua yote ya Paulo kwa Warumi. Alikuwa mmoja wa wahudumu au mdiakonia wa kike katika Kanisa la wakati huo. Yaelekea alikuwa na huduma kanisani kama wale saba waliochaguliwa na mitume (taz Mate 6:1-6); na alijali kazi yake kama Yasoni wa Thesalonike (taz Mate 17:6-9).; #16:1 Bandari mashariki ya Korintho na sehemu yote iliyoizunguka ilijulikana kama]

2Mpokeeni kwa ajili ya Bwana kama iwapasavyo watu wa Mungu. Mpeni msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, maana yeye amekuwa mwema sana kwa watu wengi na kwangu pia.

3Salamu zangu ziwafikie Priska na Akula, wafanyakazi wenzangu katika utumishi wa Kristo Yesu.[#16:3 Anaanza kumtaja Priska, yaelekea huyo alikuwa na bidii katika ufuasi wake, labda kuliko mume wake. Paulo alikwisha kutana nao huko Korintho (taz Mate 18:2). Mara mbili zaidi anatuma salamu kwao (taz 1Kor 16:19; 2Tim 4:19).; #16:3 Walimsaidia Paulo kumfundisha Apolo huko Efeso (Mate 18:24-26) na walitengeneza mahema pamoja naye (taz Mate 18:1-4).; #16:3-16 Sehemu yote ni salamu. Ni sehemu ya mwisho wa barua yake.]

4Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Wanastahili shukrani; si tu kutoka kwangu, bali pia kutoka kwa makanisa yote ya watu wa mataifa mengine.[#16:4 Haielezwi popote katika barua zake juu ya tukio hilo, bila shaka Paulo alikwisha waeleza watu na walijua ndiyo sababu hakuendelea kueleza juu yake.; #16:4 Kwa kazi waliyofanya kushirikiana naye Paulo ambaye alitumwa kwa mataifa mengine.]

5Salamu zangu pia kwa kanisa linalokutana nyumbani kwao.[#16:5 Inaonesha ya kwamba kulikuwako makanisa ndani ya nyumba za watu. Labda ilitokea hivyo kwa ajili ya upinzani wa watu wengine ili wasijenge makanisa - nyumba za kuabudia kwani Priska na Akula walivyokuwa na bidii, pamoja na wenzao wasingeweza kushindwa kujenga kanisa.]

Salamu zangu zimfikie rafiki yangu Epaineto ambaye ni wa kwanza katika mkoa wa Asia kumwamini Kristo.

6Nisalimieni Maria ambaye amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.[#16:6 Maelezo zaidi kuhusu huyu, hayapo pengine katika barua za Paulo. Katika Agano Jipya lote Maria sita wanatajwa.]

7Salamu zangu kwa Androniko na Yunia, wananchi wenzangu waliofungwa gerezani pamoja nami; wao wanajulikana sana kati ya mitume; tena walikuwa Wakristo kabla yangu mimi.[#16:7 Yaelekea hawa walikuwa Wayahudi kama Herodiana (taz aya ya 11), labda wakiwa ni miongoni mwa wale waliohamia Roma. Jina ni la kike.; #16:7 Bila shaka walihudumu na Paulo kwa muda, ingawa hakuna maelezo zaidi walivyoshirikiana pamoja kikazi.; #16:7 Kwa vyovyote hawakuwa kati ya wale kumi na wawili lakini hapa neno limetumiwa kwa kijumla kumaanisha wahudumu wanaoendeleza kazi ya mitume kama Paulo mwenyewe anavyojiita mtume (taz maelezo ya 1:1).]

8Salamu zangu kwa Ampliato, rafiki yangu katika kuungana na Bwana.[#16:8-10 Ampliato, Urbano, Staku, Apele yasemekana kuwa haya yote ni majina ambayo yalifahamika kama ya Watumwa kwani yalipatikana kati ya orodha ya watumishi wa mfalme.]

9Salamu zangu zimfikie Urbano, mfanyakazi mwenzangu katika utumishi wa Kristo; salamu zangu pia kwa rafiki yangu Staku.

10Nisalimieni Apele ambaye uaminifu wake kwa Kristo umethibitishwa. Salamu zangu kwa wote walio nyumbani mwa Aristobulo.[#16:10 Jina hili ni kama lile la mjukuu wa Herode Mkuu na ndugu yake Herode Agripa wa I, yasemekana ndiye anayetajwa hapa.]

11Salamu zangu kwa Herodiana, mwananchi mwenzangu; na kwa jamaa yote ya Narkisi iliyojiunga na Bwana.[#16:11 Yafikiriwa kuwa huenda ni Tiberia Klaudio Markisi ambaye alikuwa mtu tajiri aliyewekwa huru na mfalme wa Kiroma Tiberia.]

12Nisalimieni Trufena na Trufosa wanaofanya kazi katika utumishi wa Bwana, na rafiki yangu Persi ambaye amefanya mengi kwa ajili ya Bwana.[#16:12 Majina ya kike, labda walikuwa mapacha ndiyo sababu wakapata majina yenye mwanzo uleule au labda mmoja wa wazazi wao alikuwa na jina lenye mwanzo uleule.; #16:12 Huyu huenda alikuwa Mpersi kama si kitaifa huenda alizaliwa Persia halafu wazazi wake wakahamia Roma.]

13Nisalimieni Rufo, mtu hodari sana katika kazi ya Bwana, na mama yake ambaye ni mama yangu pia.

14Nisalimieni Asunkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.[#16:14-15 Majina ya watu hao hayatajwi mahali pengine popote na si rahisi kupata popote maelezo juu yao.]

15Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, pamoja na watu wote wa Mungu walio pamoja nao.

16Salimianeni nyinyi kwa nyinyi kwa ishara ya upendo. Salamu kwenu kutoka kwa makanisa yote ya Kristo.[#16:16 Tafsiri nyingine: kila kabila lina namna yake ya kusalimiana, makabila fulanifulani yana tabia ya kubusu wanaposalimiana mengine kupeana mkono tu wengine kuinama, n.k. Mara kwa mara Paulo anasema katika barua zake kuwa wanaopokea salamu zake wasalimiane kwa ishara fulani (taz pia 1Kor 16:20; 1Pet 5:14). Naye Yustini mfia dini (150 K.K.) anataja katika maandiko yake kuwa wakati wake watu walikuwa wakisalimiana kwa ishara maalumu (busu) wakati wa ibada.]

Mawaidha ya mwisho

17Ndugu zangu, nawasihi mwafichue wote wanaosababisha mafarakano na kuwafanya watu wengine waanguke, kinyume cha mafundisho mliyofundishwa. Jiepusheni na watu hao,[#16:17-18 Shauri la Paulo kwa Waroma kuhusu amani. Amekwisha washauri kuwa wakae kwa kushirikiana; pasitokee wa kukwaza wengine (taz 12:3-12; 13:8-14; 14:1,13-23). Kwa hiyo sasa ana hao ambao hawawezi kufuata mwenendo mwema wa Kikristo hao watatambuliwa wazi. Tatizo ni kwamba majina yao hayafahamiki naye Paulo hashauri wafanyiwe nini, bila shaka ni ili wafahamiwe na wengine na hapo mafundisho yao hayatakubaliwa na wengi hawatapotoshwa nao.]

18maana watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu, bali wanayatumikia matumbo yao wenyewe. Kwa maneno yao matamu na hotuba za kubembeleza hupotosha mioyo ya watu wanyofu.

19Kila mtu amesikia juu ya utii wenu katika mambo mema, na bila hatia kuhusu mambo mabaya.[#16:19 Hao hawafuati mafundisho ya kupotosha.; #16:19 Wajue kupambanua mema na mabaya, mafundisho yanayopatana na wito wao na yale yenye kupotosha. Ni kama alivyomshauri Timotheo (taz 1Tim 6:20-21; 2Tim 1:13; 2:23-25; 3:1-9,14-17; 4:3-5).]

20Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu.[#16:20 Katika barua nzima amekaza juu ya kuishi wote pamoja vizuri wakishirikiana kwa kuungana vipaji na kutambua umuhimu wa kazi za kila mmoja wao katika huduma ya Bwana (taz 12:3-8). Sasa mwisho anatilia mkazo jambo hilo la umoja. Kwa maneno mengine ni kwamba anarudia kwa kifupi aliyokwisha kusisitiza (taz pia Roma 2:10; 5:1; 8:6; 12:18; 14:17,19; 15:13,33).; #16:20 Ushindi kwa yule aletaye machafuko ni Mungu tu na ndiye atakayewasaidia. Bila shaka hapo anasisitiza kuwa huyo mwenye nguvu ndiye wamtegemee na kumtumikia. Paulo akikaza kuwa Mungu hatakawia ni kwa sababu walitumaini kuwa Kristo atarudi upesi (taz Fil 4:5; Ufu 1:3; 22:12).]

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

21Timotheo, mfanyakazi mwenzangu, anawasalimu. Hali kadhalika Lukio, Yasoni, na Sosipateri, wananchi wenzangu, wanawasalimu.[#16:21 Huyu alishirikiana na Paulo kufanya kazi ya Bwana. Ni hapa tu anamwita “mfanyakazi mwenzangu” (taz Mate 16:2 n.k.); mahali pengine anamwita mwanangu (taz 1 Tim 1:2,18; 2 Tim 1:2; 2:1), kama anavyomwita Tito (taz Tito 1:4) na Onesimo (taz File 1:10). Na mahali pengine anamwita “Mtu wa Mungu” (taz 1 Tim 6:11).; #16:21 Walikuwa Wayahudi ndiyo sababu anawataja .; #16:21 Hakuna habari zake mahali pengine, lakini huenda ndiye anayetajwa katika Mate 17:5-9 kuwa Thesalonike aliwasaidia Paulo na Sila kuwapa mahali pa kulala wasishambuliwe na adui zao.; #16:21 Pia hakuna habari zake huenda ni yule anayetajwa katika Mate 20:4 ya kwamba alikuwa Mberoya, mwana wa Pirho.]

22Nami Tertio, ninayeandika barua hii, nawasalimuni kwa jina la Bwana.[#16:22 Ni hapa tu jina hili linaonekana, mahali pengine katika barua za Paulo jina lake halitajwi. Ni shida kujua kama alifuatana na Paulo mara nyingi kama mwandishi wake kwani katika barua nyingine jina lake halimo. Yawezekana walikutana wakati huo na kuachana.]

23Gayo, mwenyeji wangu, pamoja na kanisa lote linalokutana kwake, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto, wanawasalimu.[#16:23 Huenda ni Tito Yusto mcha Mungu ambaye kwake Paulo alikaa alipokuwa Korintho (taz Mate 18:7; 1Kor 1:14). Gayo alisafiri na Paulo (taz Mate 19:29; 20:40). Alibatizwa naye Paulo (taz 1Kor 1:14). Yawezekana ndiye Yohane alimwandikia, (taz 3Yoh 1).; #16:23 Jina hili halipatikani mahali pengi, ni mahali pawili zaidi katika Agano Jipya yaani katika Mate 19:22; 2Tim 4:20. Alimsaidia Paulo katika huduma ya Bwana. Yaelekea alikuwa mtu mwenye madaraka katika Korintho. Wataalamu wamegundua jiwe ambalo lina maandiko; “Erasto kamishna wa kazi za umma alilipia sakafu hii.” Yawezekana ndiye huyo anayetajwa na Paulo kwa kuwa alikuwa; #16:23 Hili ni jina la Kilatini na maana yake ni “(mtoto) wa nne”. Habari zake hazionekani penginepo katika Agano Jipya.; #16:23 Baadhi ya makala zina aya 24: Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote! Amina.]

Sala ya kumsifu Mungu

25Basi, sasa na tumsifu Mungu! Yeye anaweza kuwaimarisheni katika ile Habari Njema niliyohubiri juu ya Yesu Kristo, na katika ile siri iliyofunuliwa na ambayo ilikuwa imefichika kwa karne nyinyi zilizopita.[#16:25-26 Hii ni nyongeza, bila shaka alikumbuka kitu cha kuongeza kusisitiza huduma aliyokwisha fanya hapo awali yaani kutangaza Habari Njema.; #16:25 Hii ni juu ya Yesu Kristo aliyoletea ulimwengu wokovu.; #16:25 Katika Kristo Mungu alionesha upendo wake wa kuokoa watu ambao ni kama kubwa kwa wanadamu. Naye Mungu amefunua hiyo kwa wanafunzi wake na kwa Paulo pia (taz pia Gal 1:12) na kwa wote wamwaminio Mwana wake.; #16:25 Siri haikufunuliwa kabla yake Kristo kuzaliwa. Hapo awali Mungu alitoa ahadi kuwa Shetani atashindwa (Mwa 3:15) na pia ahadi kwa Abrahamu kuwa katika yeye mataifa yote yatabarikiwa (Mwa 12:3). Pia kuwa katika Yuda mtawala atazaliwa (Mwa 49:10) na ahadi ya kuja kwa Masiha kama manabii walivyotabiri (taz k.m. Isa 7:14; 9:6,7; 11:1-5; Mika 5:2). Ahadi ya kuja kwa Mwokozi ilichukua muda mrefu, naye Paulo anaona hiyo haikuwa wazi kwa taifa lake Mungu alilochagua. Katika Kristo Maandiko yametia.]

26Lakini, sasa ukweli huo umefunuliwa kwa njia ya maandiko ya manabii; na kwa amri ya Mungu wa milele umedhihirishwa kwa mataifa yote ili wote waweze kuamini na kutii.[#16:26 Hapo Paulo habagui, anataka kukazia kama alivyokwisha sema katika barua yake kuwa wokovu ni kwa wote, wawe Wayahudi au wasio Wayahudi. Watu wa mataifa mbalimbali wakiamini na uzima wa milele ni wao.]

27Kwake Mungu aliye peke yake mwenye hekima, uwe utukufu kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele! Amina.[#16:27 Anaurudia mkazo wake kuwa hakuna mwenye hekima kama Mungu, Baba yake Yesu Kristo na Baba ya wote wamwaminio (taz 11:33).; #16:27 Sifa ya hali ya juu kuliko zote, na ni Mungu mwenye kustahili sifa hiyo (taz pia 11:36; 2Kor 3:18; 4:6; 8:23; Gal 1:5; Fil 1:11; 2:11; 2Thes 2:14; 1Tim 1:11,17; 2Tim 2:10; 4:18; Tit 2:13).]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania