Sira 17

Sira 17

1Bwana aliumba binadamu kwa udongo

na hukohuko udongoni binadamu atarudi.

2Aliwapangia binadamu siku za kuishi,[#17:2 Mwa 6:3; Zab 90:10.]

na kuwapa mamlaka juu ya vitu vyote duniani.

3Aliwapa nguvu kama zake mwenyewe,

aliwaumba kwa mfano wake.

4Alivifanya viumbe vyote vimwogope binadamu,

akawapa binadamu mamlaka juu ya wanyama na ndege.

6Aliwapa binadamu ndimi, macho na masikio,

akawapa na moyo wa kuweza kufikiri.

7Aliwajaza maarifa na akili,

akawaonesha yaliyo mema na mabaya.

8Alisimika jicho lake ndani yao,

ili kuwawezesha kuona uzuri wa kazi zake,

10wapate kulisifu jina lake takatifu,

na kutangaza ukuu wa kazi zake.

11Aliweka mbele yao elimu,

na kuwajalia sheria ya uhai.

12Alifanya nao agano la milele,

na kuwafunulia maamuzi yake.

13Macho yao yakaona utukufu wake,

na masikio yao yakasikia utukufu wa sauti yake.

14Aliwaambia, “Msifanye uovu wowote;”

akawaamuru namna ya kuishi na jirani zao.

Mungu ni Hakimu

15Bwana anaiona mienendo ya binadamu;

hawawezi kujificha mbele yake.

17Aliweka mtawala juu ya kila taifa,

lakini Israeli ni mali yake Bwana binafsi.

19Matendo yote ya watu ni wazi kwa Bwana kama jua,

kila wanachofanya anakiona mbele yake.

20Maovu ya binadamu hayawezi kufichika mbele yake,

dhambi zao ziko wazi mbele ya Bwana.

22Sadaka kwa maskini ni kama mhuri kwake,

yeye huthamini wema wa mtu kama mboni ya jicho lake.

23Baadaye atatokea na kuwalipiza waovu;

watapata kila mmoja wanachostahili.

24Lakini wale wanaotubu atawajalia wamrudie,

na huwatia moyo wale waliokata tamaa.

Wito wa toba

25Mgeukie Bwana na kuacha dhambi zako;

omba mbele yake na uache makosa yako.

26Mrudie Mungu Mkuu na kuachana na uovu;

uchukie kwa moyo wote kufanya machukizo.

27Huko kuzimu nani atamwimbia sifa Mungu Mkuu?

Ni wale tu walio hai wanaoweza kumshukuru.

28Waliokufa na wasiokuwako tena hawawezi kumsifu;

ni wale walio hai na wazima ndio wanaoweza kumsifu Bwana.

29Jinsi gani huruma ya Bwana ilivyo kuu,

na jinsi anavyowasamehe wanaomrudia!

30Sisi binadamu hatuwezi kuwa na kila kitu;

maana sisi sote ni viumbe vyenye kufa.

31Ni kitu gani king'aacho kama jua? Hata hivyo, jua nalo hupatwa.

Binadamu aliye kiumbe hufikiria tu maovu.

32Bwana hulikagua jeshi lote la mbinguni,

lakini binadamu ni mavumbi tu na majivu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania