Tobiti 1

Tobiti 1

1Hizi ni habari za maisha ya Tobiti mwana wa Tobieli, mwana wa Ananieli, mwana wa Adueli, mwana wa Gabaeli, wa ukoo wa Asieli, wa kabila la Naftali.[#1:1 Kadiri ya tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX), jina la baba ni Tobiti na mwanawe aliitwa Tobia. Tafsiri ya Kilatini wote baba na mtoto wana jina Tobia. Kwa sababu hiyo kitabu chenyewe kinajulikana pia kama kitabu cha Tobia. Tobiti alikuwa mtoto wa Tobieli.; #1:1 Mababu wote ambao wanamuunganisha Tobiti na Naftali walichukua majina yaliyoundwa pamoja na neno “-el” (Kwa Kiebrania “Mungu”), jambo ambalo linadhihirisha kwamba mwandishi alitaka kuonesha kwamba familia hiyo ilikuwa yenye dini sana. Eneo la Naftali lilikuwa katika Galilaya (taz aya 2).]

2Wakati Shalmanesa alipokuwa mfalme wa Ashuru, Tobiti alichukuliwa uhamishoni kutoka mji wa Thisbe ulioko kusini mwa Kadeshi huko Naftali kaskazini mwa Galilaya, magharibi-kaskazini mwa mji wa Hazori na kaskazini mwa Shefati.[#1:2 Au, “Sargoni” (rejea aya ya 15). Alikuwa mwanawe Tiglath-pileseri na alitawala baada yake. Kadiri ya 2Fal 15:29 yeye ndiye aliyeuteka mji wa Samaria, mji mkuu wa Israeli, akasafirisha kundi kubwa la watu na kuwahamishia nchini Ashuru (yapata mwaka 734-732 K.K.).; #1:2 Haufahamiki dhahiri mahali mji huu ulipokuwa.; #1:2 Miji inayotajwa hapa ilikuwa kaskazini mwa Galilaya.]

Maisha ya ujana ya Tobiti

3Mimi Tobiti nimefuata njia za haki na kutenda mema maisha yangu yote. Mara nyingi niliwasaidia jamaa na Wayahudi wenzangu maskini waliohamishiwa pamoja nami huko Ninewi, nchini Ashuru.

4Nilipokuwa kijana nikiwa bado nyumbani nchini Israeli, makabila yote katika Israeli yaliwajibika kwenda kutoa sadaka Yerusalemu. Yerusalemu ulikuwa ndio mji pekee ambao Mungu alikuwa ameuteua miongoni mwa miji yote ya Israeli uwe mahali pa kutolea tambiko zao; huko ndiko kulikojengwa hekalu ambalo ni makao yake matakatifu na ya kudumu. Lakini kabila langu lote la Naftali lilijitenga na mji wa Yerusalemu na ukoo wa Daudi.[#1:4 Kinachosemwa hapa ni ukumbusho wa wakati ule ambapo utawala wa Daudi ulikuwa umegawanyika sehemu mbili (1Fal 12:16-20).]

5Ndugu zangu wote na ukoo wa Naftali walitambikia juu ya kila kilima kwa ile sanamu ya ndama aliyoifanya Yeroboamu mfalme wa Israeli huko Dani katika mkoa wa Galilaya.

Tobiti azingatia dini yake

6Katika jamaa yangu ni mimi peke yangu niliyekwenda kuabudu mara kwa mara huko Yerusalemu kutekeleza sheria inayowabana watu wote wa Israeli milele. Niliharakisha kwenda Yerusalemu na sehemu ya mazao ya kwanza ya mavuno na wanyama, zaka za mifugo na manyoya ya kwanza ya kondoo.

7Vitu hivi niliwapa makuhani, wazawa wa Aroni, kwa ajili ya madhabahu. Niliwapa Walawi waliohudumu huko Yerusalemu zaka yangu ya divai, ngano, zeituni, makomamanga na matunda mengine. Kwa miaka sita mfululizo nilichukua fedha ya zaka na kuilipa huko Yerusalemu.

8Sehemu ya tatu ya zaka niliwapa yatima, wajane na wageni walioishi miongoni mwa watu wa Israeli; niliwapelekea kama zawadi kila miaka mitatu. Tulipokula chakula tulifanya kulingana na Sheria ya Mose na mawaidha ya Debora mama wa babu yangu Ananieli. Baba yangu alikuwa amekufa akaniacha yatima.

Uaminifu wa Tobiti uhamishoni

9Mara nilipokuwa mtu mzima nilimwoa Ana, mwanamke wa kabila langu. Tulijaliwa mtoto tukamwita Tobia.[#1:9 Rejea 1:1 maelezo.]

10Baadaye nilichukuliwa mateka na kupelekwa Ninewi.

Tulipokuwa tunakaa Ninewi jamaa zangu na Wayahudi wenzangu wote walikuwa wakila chakula walichokula wale watu wasio Wayahudi,

11lakini mimi nilikataa kula chakula hicho.

12Kwa kuwa nilizishika kwa moyo amri za Mungu aliye juu,

13Mungu alimfanya mfalme Shalmanesa anipendelee na kunijali, hata nikapewa madaraka ya kumnunulia mfalme chakula chake.

14Kabla mfalme huyo hajafariki, nilikwenda mara nyingi nchini Media kumnunulia vitu. Siku moja, nilipokuwa mjini Rage huko Media, nilimwachia Gabaeli, nduguye Gabria, fedha mifuko kadhaa, nikamwomba anitunzie. Ndani ya mifuko hiyo mlikuwa na sarafu za shaba zaidi ya kilo 300.[#1:14 Hiyo ilikuwa nchi iliyokuwa upande wa mashariki wa Palestina; kwa sasa eneo hilo ni nchi ya Irani.; #1:14 Neno kwa neno, “talanta kumi”.]

15Shalmanesa alipofariki, Senakeribu, mwanawe, alitawala mahali pake. Mara yakazuka majambazi huko na huko katika barabara za Media, nami nikashindwa kwenda tena Media.[#1:15 Shalmanase V alipokufa (mwaka 722 K.K.) waliotawala baada yake walikuwa kaka yake Sargoni II (ambaye hatajwi hapa au katika II Fal 17) kisha mwanawe Senakeribu (705-681 K.K.).]

Tobiti azika wafu

16Shalmanesa alipokuwa bado anatawala, niliwasaidia sana Wayahudi wenzangu maskini.

17Wenye njaa, niliwapatia chakula changu na kuwapa nguo wale waliotindikiwa nazo. Kila nilipokuta maiti ya mmoja wa watu wangu ametupwa nje ya ukuta wa mji, nilimwokota na kumzika kwa heshima.[#1:17 Kuacha mtu bila kumzika ilichukuliwa kuwa ni kitendo kibaya mno cha utovu wa heshima (Yer 16:14; Eze 29:5). Kwa hiyo ilikuwa ni wajibu mtakatifu kuwazika wafu vizuri (rejea 2Sam 2:4-5; Sira 38:16-17). Umuhimu wa jambo hili unatiliwa mkazo katika kitabu cha Tobiti. Rejea pia 2:3-8; 12:12-13.]

18Mfalme Senakeribu alipomuua mtu yeyote aliyekimbilia nchini mwake kutoka Yudea, mimi nilimzika kwa siri. Mfalme aliwaua watu wengi kutuliza hasira yake. Baadaye alipozitafuta maiti hizo hakuzipata.

19Halafu mtu mmoja wa Ninewi alimwarifu mfalme kwamba mimi ndiye niliyekuwa nikiwazika Waisraeli waliouawa. Nilipogundua kuwa mfalme alipata kujua habari zangu zote, na nilipoona mimi mwenyewe watu wakinitafuta kuniua niliingiwa na hofu na kutoroka.

20Mali yangu yote ikataifishwa na kuwekwa katika hazina ya mfalme. Nilibakiwa tu na mke wangu Ana na mwanangu Tobia.

Tobiti aokolewa na binamu yake

21Ilipokuwa bado hata hazijapita siku hamsini wana wawili wa Senakeribu walimuua baba yao, wakakimbilia kwenye milima ya Ararati. Esar-hadoni, mwana mwingine wa Senakeribu, akawa mfalme; akamteua Ahika, mwana wa ndugu yangu Anaeli, awe waziri wa fedha na mratibu wa mambo yote ya utawala.[#1:21 Mwandishi anamtaja hapa mtu mmoja maarufu katika maandisi na hadithi za Mashariki ya Kati ya Kale ambaye alikuwa mwenye mshauri mwenye hekima wa wafalme wa Ashuru. Hapa anaonekana kama mwana wa ndugu yake Tobiti. Taz pia 2:10; 11:19; 14:10.]

22Basi, Ahika alinitetea, nikaruhusiwa kurudi Ninewi. Hii ilikuwa mara ya pili Ahika kuwa na cheo hicho, maana alikwisha kuwa mhudumu mkuu wa divai, waziri wa fedha, mhasibu na mwangalizi wa mhuri wa ofisi chini ya mfalme Senakeribu, naye Esar-hadoni akamthibitisha katika madaraka hayo. Ahika alikuwa binamu yangu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania