2 Wakorintho 2

2 Wakorintho 2

1Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi.

2Kwa kuwa nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha?

3Niliwaandikia hivyo ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao walipaswa kunifurahisha. Nilikuwa na uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu.

4Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana moyoni mwangu, tena kwa machozi mengi; shabaha yangu haikuwa niwahuzunishe, bali niwaoneshe kina cha upendo wangu kwenu.

Msamaha kwa mwenye dhambi

5Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote. Nasema hivi ili nisiwe mkali kupita kiasi.

6Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha.

7Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi.

8Kwa hiyo, nawasihi mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwake.

9Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo.

10Mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,

11ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatujakosa kuzijua hila zake.

Wasiwasi wa Paulo huko Troa

12Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Kristo na kukuta kwamba Bwana alikuwa amenifungulia mlango,

13bado nilikuwa sina amani kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao, nikaenda Makedonia.

14Lakini Mungu apewe shukrani, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye.

15Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea.

16Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo?

17Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na neno la Mungu ili tujifaidishe. Bali tunalinena neno lake kwa unyofu katika Kristo tukiwa mbele za Mungu, kama watu waliotumwa na Mungu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.