Ezekieli 3

Ezekieli 3

1Naye akaniambia, “Mwanadamu, kula kilichoko mbele yako, kula kitabu hiki, kisha uende ukaseme na nyumba ya Israeli.”

2Hivyo, nikafungua kinywa changu, naye akanipa kile kitabu nikile.

3Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, kula kitabu hiki ninachokupa, ujaze tumbo lako.” Kwa hiyo nikaula, nao ulikuwa mtamu kama asali kinywani mwangu.

4Kisha akaniambia, “Mwanadamu, sasa nenda katika nyumba ya Israeli ukawanenee maneno yangu.

5Hukutumwa kwa taifa lenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli.

6Sikukutuma kwa mataifa mengi yenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu ambao maneno yao hutayaelewa. Hakika ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza.

7Lakini nyumba ya Israeli haitakusikiliza, kwa kuwa hawako radhi kunisikiliza mimi, kwa kuwa nyumba yote ya Israeli ni wenye paji gumu na mioyo ya ukaidi.

8Tazama, nimefanya uso wako mgumu dhidi ya nyuso zao, na paji la uso wako gumu dhidi ya paji za nyuso zao.

9Kama vile almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyolifanya paji la uso wako. Usiwaogope wala usiwahofu, ijapokuwa ni nyumba ya uasi.”

10Naye akaniambia, “Mwanadamu, sikiliza kwa makini na uyatie moyoni mwako maneno yote nitakayosema nawe.

11Kisha nenda kwa watu wa taifa lako walio uhamishoni, ukaseme nao. Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi’; iwe watasikiliza au hawatasikiliza.”

12Ndipo Roho akaniinua juu, nami nikasikia sauti kubwa ya ngurumo nyuma yangu ikisema, “Utukufu wa Bwana na utukuzwe katika makao yake!”

13Ilikuwa ni sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yakigusana moja kwa lingine, na sauti ya magurudumu kando yao, sauti kubwa ya ngurumo.

14Kisha Roho akaniinua juu na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na hasira moyoni mwangu, nao mkono wenye nguvu wa Bwana ukiwa juu yangu.

15Nikafika kwa wale watu waliokuwa uhamishoni huko Tel-Abibu karibu na Mto Kebari. Nikakaa miongoni mwao kwa muda wa siku saba, nikiwa nimejawa na mshangao.

Onyo kwa Israeli

16Mwishoni mwa hizo siku saba neno la Bwana likanijia kusema:

17“Mwanadamu, nimekufanya uwe mlinzi wa nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo, ukawape onyo litokalo kwangu.

18Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usimwonye mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu akifa katika dhambi yake, damu yake nitaidai mkononi mwako.

19Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako.

20“Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako.

21Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.”

22Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu huko, naye akaniambia, “Simama uende sehemu tambarare, nami nitasema nawe huko.”

23Kwa hiyo niliinuka nikaenda mahali tambarare. Utukufu wa Bwana ulikuwa umesimama huko, kama utukufu ule niliouona kando ya Mto Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.

24Ndipo Roho akaja ndani yangu, akanisimamisha kwa miguu yangu. Akasema nami akaniambia: “Nenda ukajifungie ndani ya nyumba yako.

25Nawe, ee mwanadamu, watakufunga kwa kamba; utafungwa ili usiweze kuwaendea watu.

26Nitaufanya ulimi wako ushikamane kwenye kaakaa la kinywa chako, ili uwe kimya usiweze kuwakemea, kwa kuwa wao ni nyumba ya uasi.

27Lakini nitakaposema nawe, nitafungua kinywa chako nawe utawaambia, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi.’ Yeyote atakayesikiliza na asikilize, na yeyote atakayekataa na akatae; kwa kuwa wao ni nyumba ya uasi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.