Ayubu 5

Ayubu 5

Elifazi anaendelea

1“Itana, ukitaka, lakini ni nani atakayekujibu?

Ni yupi kati ya hao watakatifu utakayemgeukia?

2Kuweka uchungu moyoni humuua mpumbavu,

nao wivu humchinja mjinga.

3Mimi mwenyewe nimemwona mpumbavu akistawi,

lakini ghafula nyumba yake ikawa imelaaniwa.

4Watoto wake wako mbali na usalama,

hushindwa mahakamani bila mtetezi.

5Wenye njaa huyala mavuno yake,

wakiyatoa hata katikati ya miiba,

nao wenye kiu huitamani sana mali yake.

6Kwa maana taabu haioti kutoka kwa udongo,

wala ubaya hauchipui kutoka ardhini.

7Lakini mwanadamu huzaliwa ili kutaabika,

kwa hakika kama cheche za moto zinavyoruka kuelekea juu.

8“Lakini ingekuwa ni mimi, ningemlalamikia Mungu,

ningeweka shauri langu mbele zake.

9Yeye hutenda maajabu yasiyoweza kutambuliwa,

miujiza isiyoweza kuhesabika.

10Yeye huipa nchi mvua,

huyapeleka maji kunyesha mashamba.

11Huwainua juu wanyonge,

nao wale wanaoomboleza

huinuliwa wakawa salama.

12Huipinga mipango ya wenye hila,

ili mikono yao isifikie ufanisi.

13Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao,

nayo mipango ya wadanganyifu huifagilia mbali.

14Giza huwapata wakati wa mchana;

wakati wa adhuhuri hupapasa kama vile usiku.

15Humwokoa mhitaji kutokana na upanga ulioko kinywani mwao;

huwaokoa kutokana na makucha ya wenye nguvu.

16Kwa hiyo maskini analo tarajio,

nao udhalimu hufumba kinywa chake.

17“Heri mtu yule ambaye Mungu humkanya;

kwa hiyo usidharau adhabu yake Mwenyezi.

18Kwa kuwa hutia jeraha, lakini pia huyafunga;

huumiza, lakini mikono yake pia huponya.

19Kutoka majanga sita atakuokoa;

naam, hata katika saba hakuna dhara litakalokupata wewe.

20Wakati wa njaa atakukomboa wewe na kifo,

naye katika vita atakukomboa na pigo la upanga.

21Utalindwa kutokana na kichapo cha ulimi,

wala hutakuwa na sababu ya kuogopa maangamizi yatakapokujia.

22Utayacheka maangamizi na njaa,

wala hutakuwa na sababu ya kuwaogopa

wanyama wakali wa mwituni.

23Kwa kuwa utakuwa na agano na mawe ya mashamba,

nao wanyama pori watakuwa na amani nawe.

24Utajua kwamba hema lako li salama;

utahesabu mali yako wala hutakuta chochote kilichopungua.

25Utajua kuwa watoto wako watakuwa wengi,

nao wazao wako wengi kama majani ya nchi.

26Utaingia kaburini ukiwa na umri wa uzee mtimilifu,

kama masuke ya ngano yanapokusanywa kwa wakati wake.

27“Tumelichunguza hili, nalo ni kweli.

Hivyo lisikie na ulitendee kazi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.