Mathayo 11

Mathayo 11

Yesu na Yohana Mbatizaji

(Lk 7:18‑35)

1Baada ya Yesu kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji ya Galilaya.

2Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake[#11:2 maana yake Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.]

3ili wakamuulize, “Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

4Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona:

5Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema.

6Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

7Wale wanafunzi wa Yohana walipokuwa wanaondoka, Yesu akaanza kusema na umati wa watu kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipoenda kule nyikani, mlienda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?

8Kama sivyo, mlienda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha! Watu wanaovaa mavazi ya kifahari wako katika majumba ya wafalme.

9Basi mlienda kuona nini? Mlienda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.

10Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

“ ‘Tazama nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako.’

11Amin, nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji. Lakini aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko Yohana.

12Tangu siku za Yohana Mbatizaji hadi sasa, ufalme wa mbinguni hunyakuliwa kwa nguvu, nao wenye nguvu wanauteka.

13Kwa maana manabii wote na Sheria walitabiri hadi wakati wa Yohana.

14Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye ndiye yule Eliya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja.

15Yeye aliye na masikio, na asikie.

16“Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,

17“ ‘Tuliwapigia filimbi,

lakini hamkucheza;

tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,

lakini hamkuomboleza.’

18Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’

19Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.”

Onyo kwa miji isiyotubu

(Lk 10:13‑15)

20Ndipo Yesu akaanza kuishutumu miji ambayo alifanya miujiza yake mingi, kwa maana watu wake hawakutubu.

21“Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.

22Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi.

23Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha! Utashushwa hadi Kuzimu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungekuwepo hadi leo.[#11:23 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades , yaani mahali pa wafu.]

24Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”

Hakuna amjuaye Baba ila Mwana

(Lk 10:21‑22)

25Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo.

26Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

27“Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

Yesu awaita waliolemewa na mizigo

28“Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha katika nafsi zenu.

30Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.