Mathayo 26

Mathayo 26

Kufa na kufufuka kwa Yesu

Njama ya kumuua Yesu

(Mk 14:1‑2; Lk 22:1‑2; Yn 11:45‑53)

1Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake,

2“Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.”

3Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa.

4Wakapanga kumkamata Yesu kwa siri na kumuua.

5Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.”

Yesu apakwa mafuta huko Bethania

(Mk 14:3‑9; Lk 7:35-38; Yn 12:1‑8)

6Yesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma.

7Naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa. Akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.

8Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini?

9Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.”

10Yesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana.

11Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.

12Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu.

13Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”

Yuda akubali kumsaliti Yesu

(Mk 14:10‑11; Lk 22:3‑6)

14Kisha mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alienda kwa viongozi wa makuhani

15na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha.

16Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu.

Yesu ala Pasaka na wanafunzi wake

(Mk 14:12‑21; Lk 22:7‑23; Yn 13:21‑30)

17Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”

18Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ”

19Hivyo wanafunzi wakafanya vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.

20Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili.

21Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”

23Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti.

24Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!”

25Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?”

Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”

Kuanzishwa kwa meza ya Bwana

(Mk 14:22‑26; Lk 22:14‑20; 1Kor 11:23‑25)

26Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”

27Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki.

28Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.

29Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”

30Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.

Yesu atabiri kuwa Petro atamkana

(Mk 14:27‑31; Lk 22:31‑34; Yn 13:31‑38)

31Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:

“ ‘Nitampiga mchungaji,

nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’

32Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

33Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”

34Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

35Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Yesu aomba katika Bustani ya Gethsemane

(Mk 14:32‑42; Lk 22:39‑46)

36Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake hadi kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.”

37Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika.

38Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

39Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

40Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja?

41Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”

42Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”

43Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito.

44Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.

45Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.

46Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”

Yesu akamatwa

(Mk 14:43‑50; Lk 22:47‑53; Yn 18:1‑11)

47Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.

48Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.”

49Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu.

50Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”

Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu.

51Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.

52Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako alani mwake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga.

53Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?

54Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”

55Wakati huo, Yesu akaambia wale umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata?

56Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.

Yesu mbele ya Baraza la Wayahudi

(Mk 14:53‑65; Lk 22:54‑71; Yn 18:13‑24)

57Wale waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika.

58Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.

59Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua.[#26:59 ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.]

60Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.

Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo

61na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”

62Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”

63Lakini Yesu akakaa kimya.

Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”

64Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia alivyokufuru.

66Uamuzi wenu ni gani?”

Wakajibu, “Anastahili kufa.”

67Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi

68na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

Petro amkana Yesu

(Mk 14:66‑72; Lk 22:56‑62; Yn 18:15‑18, 25‑27)

69Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mjakazi mmoja akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”

70Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”

71Alipotoka nje kufika kwenye lango, mjakazi mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.”

72Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”

73Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”

74Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”

Papo hapo jogoo akawika.

75Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.