The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Musa,
2“Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Baada ya ninyi kuingia katika nchi ninayowapa kama nyumbani,
3nanyi mkitoa sadaka za kuteketezwa kwa moto, kutoka makundi ya ngʼombe au kondoo, kama harufu nzuri inayompendeza Bwana , ikiwa ni sadaka za kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum ama sadaka ya hiari au sadaka ya sikukuu zenu,
4ndipo yeye aletaye sadaka yake ataiweka mbele za Bwana sadaka ya nafaka, sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta.[#15:4 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na kilo moja.; #15:4 Robo ya hini ni sawa na lita moja.]
5Pamoja na kila mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, andaa robo ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji.
6“ ‘Pamoja na kondoo dume, andaa sadaka ya nafaka ya sehemu mbili za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na theluthi moja ya hini ya mafuta,[#15:6 Sehemu mbili za kumi ya efa ni sawa na kilo 2.; #15:6 Theluthi moja ya hini ni sawa na lita moja na nusu.]
7na theluthi moja ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Vitoe kama harufu nzuri inayompendeza Bwana .
8“ ‘Unapoandaa fahali mchanga kama sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum au sadaka ya amani kwa Bwana ,
9leta pamoja na huyo fahali sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi ya efa uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.[#15:9 Sehemu tatu za kumi ya efa ni sawa na kilo 3.; #15:9 Nusu ya hini ni sawa na lita 2.]
10Pia utaleta nusu ya hini ya divai kuwa sadaka ya kinywaji. Itakuwa sadaka iliyoteketezwa kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Bwana .
11Kila fahali au kondoo dume, kila mwana-kondoo au mbuzi mchanga, atatayarishwa kwa njia hii.
12Fanyeni hivi kwa ajili ya kila mmoja, kwa kadiri ya wingi wa mtakavyoandaa.
13“ ‘Kila mmoja ambaye ni mzawa ni lazima afanye vitu hivi kwa njia hii hapo aletapo sadaka ya kuteketezwa kwa moto kama harufu nzuri inayompendeza Bwana .
14Kwa vizazi vijavyo, wakati wowote mgeni au mtu mwingine yeyote anayeishi miongoni mwenu aletapo sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Bwana , ni lazima afanye sawasawa kabisa na jinsi mnavyofanya ninyi.
15Jumuiya itakuwa na sheria hizo hizo kwenu na kwa mgeni aishiye miongoni mwenu; hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Ninyi na mgeni mtakuwa sawa mbele za Bwana :
16Sheria hizo na masharti hayo vitawahusu ninyi na pia mgeni aishiye miongoni mwenu.’ ”
17Bwana akamwambia Musa,
18“Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapeleka,
19nanyi mkala chakula cha nchi hiyo, toeni sehemu ya chakula hicho kuwa sadaka kwa Bwana .
20Toeni andazi kutoka kwa malimbuko ya chakula chenu kitokacho katika ardhi, na mkitoe kama sadaka kutoka sakafu ya kupuria nafaka.
21Kwa vizazi vyote vijavyo hamna budi kutoa sadaka hii kwa Bwana kutoka kwa malimbuko ya unga wenu.
22“ ‘Basi kama pasipo kukusudia umeshindwa kushika mojawapo katika amri hizi ambazo Bwana alimpa Musa,
23amri yoyote ya Bwana kwenu kupitia Musa, tangu siku ile Bwana alipowapa na inaendelea hadi vizazi vyote vijavyo;
24ikiwa hili limefanyika pasipo kukusudia bila jumuiya kuwa na habari nalo, basi jumuiya yote itatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa ikiwa harufu nzuri inayompendeza Bwana , pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji zilizoamriwa kwayo, na beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
25Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Waisraeli, nao watasamehewa, kwa kuwa haikuwa makusudi nao wamemletea Bwana sadaka iliyoteketezwa kwa moto na sadaka ya dhambi kwa ajili ya kosa lao.
26Jumuiya yote ya Waisraeli pamoja na wageni wanaoishi miongoni mwao watasamehewa, kwa sababu watu wote walihusika katika kosa lile lisilokusudiwa.
27“ ‘Lakini kama mtu mmoja peke yake akitenda dhambi pasipo kukusudia, ni lazima alete mbuzi jike wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
28Kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya yule aliyekosa kwa kufanya dhambi pasipo kukusudia, upatanisho utakapofanywa kwa ajili yake, atasamehewa.
29Sheria hiyo moja itamhusu kila mmoja ambaye ametenda dhambi pasipo kukusudia, awe Mwisraeli mzawa ama mgeni.
30“ ‘Lakini yeyote ambaye amefanya dhambi kwa dharau awe mzawa au mgeni, anamkufuru Bwana , naye mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
31Kwa sababu amelidharau neno la Bwana na kuvunja amri zake, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali; hatia yake inabaki juu yake.’ ”
32Waisraeli walipokuwa jangwani, mtu mmoja alikutwa akikusanya kuni siku ya Sabato.
33Wale waliomkuta akikusanya kuni wakamleta kwa Musa, na Haruni na kusanyiko lote,
34nao wakamweka kifungoni, kwa sababu haikufahamika kwa wazi kwamba afanyiwe nini.
35Ndipo Bwana akamwambia Musa, “Huyo mtu ni lazima afe. Kusanyiko lote lazima wampige mawe nje ya kambi.”
36Hivyo kusanyiko wakamtoa nje ya kambi na kumpiga mawe hadi akafa, kama Bwana alivyomwamuru Musa.
37Bwana akamwambia Musa,
38“Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo.
39Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote za Bwana , ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu.
40Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu.
41Mimi Ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa Misri niwe Mungu wenu. Mimi Ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”