Hesabu 27

Hesabu 27

Binti za Selofehadi

1Binti za Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, walikuwa wa koo za Manase mwana wa Yusufu. Majina ya hao binti yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Walikaribia

2ingilio la Hema la Kukutania na kusimama mbele ya Musa, kuhani Eleazari, viongozi na kusanyiko lote, wakasema,

3“Baba yetu alikufa jangwani. Hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora, ambao walifungamana pamoja dhidi ya Bwana , lakini alikufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe na hakuacha wana.

4Kwa nini jina la baba yetu lifutike kutoka ukoo wake kwa sababu hakuwa na mwana? Tupatie milki miongoni mwa ndugu za baba yetu.”

5Kwa hiyo Musa akaleta shauri lao mbele za Bwana ,

6naye Bwana akamwambia Musa,

7“Wanachosema binti za Selofehadi ni sawa. Ni lazima kwa hakika uwape milki kama urithi miongoni mwa ndugu za baba yao, na kubadili urithi wa baba yao uwe wao.

8“Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake.

9Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake.

10Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake.

11Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama Bwana alivyomwamuru Musa.’ ”

Yoshua kuchukua nafasi ya Musa

(Kum 31:1‑8)

12Kisha Bwana akamwambia Musa, “Kwea mlima huu katika safu za Abarimu uione nchi ninayowapa Waisraeli.

13Baada ya kuiona, wewe pia utakusanywa pamoja na watu wako kama ndugu yako Haruni alivyokusanywa,

14kwa kuwa jumuiya ilipoasi amri yangu kwenye maji katika Jangwa la Sini, wakati jumuiya ilipogombana nami, nyote wawili mliacha kuitii amri yangu ya kuniheshimu kama mtakatifu mbele ya macho yao.” (Haya yalikuwa maji ya Meriba huko Kadeshi, katika Jangwa la Sini.)

15Musa akamwambia Bwana ,

16“Bwana , Mungu wa roho zote za wanadamu, na amteue mtu juu ya jumuiya hii

17ili atoke na kuingia mbele yao, atakayewaongoza katika kutoka kwao na kuingia kwao, ili watu wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.”

18Kwa hiyo Bwana akamwambia Musa, “Mchukue Yoshua mwana wa Nuni, mtu ambaye Roho yuko ndani yake, uweke mkono juu yake.

19Msimamishe mbele ya kuhani Eleazari pamoja na kusanyiko lote, umpe maagizo mbele yao.

20Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli wapate kumtii.

21Atasimama mbele ya kuhani Eleazari, ambaye atapokea maamuzi kwa ajili yake, kwa kuuliza mbele za Bwana kwa Urimu. Kwa amri yake, yeye na jumuiya yote ya Waisraeli watatoka, na kwa amri yake, wataingia.”[#27:21 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.]

22Musa akafanya kama Bwana alivyomwagiza. Akamtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na kusanyiko lote.

23Kisha akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Yoshua na kumpa maagizo, kama vile Bwana alivyoelekeza kupitia kwa Musa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.