Zekaria 14

Zekaria 14

Bwana yuaja kutawala

1Siku ya Bwana inakuja ambayo nyara zilizotekwa kwenu zitagawanywa miongoni mwenu.

2Nitayakusanya mataifa yote huko Yerusalemu kupigana dhidi yake, mji utatekwa, nyumba zitavamiwa na kuporwa na wanawake watanajisiwa. Nusu ya mji wataenda uhamishoni, lakini watakaobaki hawataondolewa kutoka mjini.

3Kisha Bwana atatoka na kupigana dhidi ya watu wa yale mataifa, kama apiganavyo siku ya vita.

4Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, mashariki mwa Yerusalemu, nao Mlima wa Mizeituni utagawanyika mara mbili kuanzia mashariki hadi magharibi, ukifanya bonde kubwa, nusu ya mlima ukisogea kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini.

5Nanyi mtakimbia kupitia katika bonde hilo la mlima wangu kwa kuwa litaenea hadi Aseli. Mtakimbia kama mlivyokimbia tetemeko la ardhi katika siku za Uzia mfalme wa Yuda. Kisha Bwana Mungu wangu atakuja na watakatifu wote pamoja naye.

6Siku hiyo hakutakuwa na nuru, baridi wala theluji.

7Itakuwa siku ya kipekee, isiyo na mchana wala usiku, siku ijulikanayo na Bwana . Jioni inapofika nuru itakuwepo.

8Siku hiyo, maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu, nusu kwenda kwenye bahari ya mashariki, na nusu kwenda kwenye bahari ya magharibi wakati wa kiangazi na wakati wa masika.[#14:8 yaani Bahari ya Chumvi au Bahari Mfu; #14:8 yaani Bahari ya Mediterania]

9Bwana atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo atakuwa Bwana mmoja, na jina lake litakuwa jina pekee.

10Nchi yote kuanzia Geba, kaskazini mwa Yuda, hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itakuwa kama Araba. Lakini Yerusalemu utainuliwa juu na kubaki mahali pake, toka Lango la Benyamini hadi mahali pa Lango la Kwanza, mpaka kwenye Lango la Pembeni na kutoka Mnara wa Hananeli hadi kwenye mashinikizo ya divai ya mfalme.[#14:10 yaani Nchi tambarare]

11Utakaliwa na watu, kamwe hautaharibiwa tena, Yerusalemu utakaa salama.

12Hii ndiyo tauni ambayo Bwana atapiga nayo mataifa yote ambayo yalipigana dhidi ya Yerusalemu: Nyama ya miili yao itaoza wangali wamesimama kwa miguu yao, macho yao yataoza kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza vinywani mwao.

13Katika siku hiyo Bwana atawatia wanaume hofu kuu. Kila mwanaume atakamata mkono wa mwenzake nao watashambuliana.

14Yuda pia atapigana katika Yerusalemu. Utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka Yerusalemu utakusanywa, wingi wa dhahabu, fedha na mavazi.

15Tauni ya aina hiyo hiyo itapiga farasi na nyumbu, ngamia na punda, nao wanyama wote walio kwenye kambi za adui.

16Kisha walionusurika katika mataifa yote ambayo yaliushambulia Yerusalemu watakuwa wakipanda Yerusalemu kila mwaka kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi na kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.

17Ikiwa taifa lolote la dunia hawataenda Yerusalemu kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, mvua haitanyesha kwao.

18Ikiwa watu wa Misri nao hawataenda kushiriki, hawatapata mvua. Bwana ataleta juu yao tauni ambayo itayapiga mataifa ambayo hayataenda kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.

19Hii itakuwa adhabu ya Misri na adhabu ya mataifa yote yale ambayo hayataenda Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.

20Katika siku hiyo, kengele zilizofungwa kwenye farasi zitaandikwa maneno haya: “Takatifu kwa Bwana ”. Navyo vyungu vya kupikia katika nyumba ya Bwana vitakuwa kama bakuli takatifu mbele ya madhabahu.

21Kila chungu kilicho Yerusalemu na Yuda kitakuwa kitakatifu kwa Bwana wa majeshi, na wote wanaokuja kutoa dhabihu watachukua baadhi ya vyungu hivyo na kupikia. Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyabiashara katika nyumba ya Bwana wa majeshi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.