The chat will start when you send the first message.
1Yonathani akaona ya kuwa sasa ndio wakati wa kufaa, akachagua watu akawapeleka Rumi ili kuuthibitisha urafiki waliokuwa nao na kuufanya upya.
2Vile vile alipeleka barua kwa Wasparta na mahali pengine.
3Wakafika Rumi, wakaingia barazani wakasema, Yonathani, kuhani mkuu, na taifa la Wayahudi wametutuma kwenu ili kuwafanyia upya ule urafiki na ushirika wa zamani.
4Wakawapa barua kwa watu kila mahali, ili wasafirishwe kwa amani kwenye nchi ya Yuda.
5Hii ndiyo nakala ya barua Yonathani aliyoiandika kwa Wasparta;
6Yonathani, kuhani mkuu, na baraza la Wayahudi, na makuhani, na watu wengine, kwa ndugu zao Wasparta, salamu.
7Hata kabla ya wakati huu barua zililetwa kwa kuhani mkuu Oniasi kutoka kwa Ariusi, aliyekuwa mfalme wenu wakati ule, kutuarifu ya kuwa tu jamaa zenu, kama inavyooneshwa katika nakala tunayoileta.
8Oniasi akamkaribisha kwa heshima yule mtu aliyetumwa akazipokea zile barua zenye habari za ushirika na urafiki.
9Sisi hatuna haja ya mambo hayo, kwa sababu msaada wetu hasa ndio vitabu vitakatifu tulivyo navyo;
10lakini tumeona vema kutuma watu kwenu ili tuuamshe udugu wetu na urafiki wetu kwenu, wala tusifarakane nanyi zaidi, maana ni wakati mwingi sana tangu mlipompeleka mjumbe kwetu.
11Sisi tunawakumbuka daima, sikukuu zetu na wakati mwingine ufaao, katika dhabihu tutoazo na katika sala zetu, kama inavyotupasa kuwakumbuka ndugu zetu;
12tena, tunaufurahia utukufu wenu.
13Lakini shida nyingi na vita vingi vilitusonga, na wafalme wanaotuzunguka walipigana nasi;
14basi, hatukutaka kuwasumbua ninyi na rafiki zetu wengine kwa habari za vita hivyo.
15Maana msaada wetu ni ule utokao mbinguni, nasi tumelindwa na adui zetu, nao adui wameshushwa.
16Tumewachagua Numenio mwana wa Antioko na Antipateri mwana wa Yasoni, tukawapeleka kwa Warumi kuufanya upya ushirika na urafiki tuliokuwa nao kwao.
17Tumewaagiza wafike kwenu pia ili kuwasalimu na kuwapeni barua yetu juu ya kufanya upya udugu wetu.
18Tafadhali utuletee jibu juu ya hayo.
19Hii ndiyo nakala ya barua Wasparta waliyomletea Oniasi:
20Ariusi, mfalme wa Wasparta, kwa Oniasi, kuhani mkuu, salamu.
21Imeonekena katika maandishi fulani ya kuwa Wasparta na Wayahudi ni jamaa, na wa ukoo wa Abrahamu.
22Madhali tumejua haya, tafadhali utuandikie habari zenu.
23Nasi tunawaandikieni kwamba wanyama wetu na mali yetu ni yenu, na yenu ni yetu. Basi, tumewaagiza wawaelezeni hayo.
24Yonathani akasikia kama majemadari wa Demetrio wamekuja tena na jeshi kubwa zaidi kuliko lile la kwanza, tayari kupigana naye.
25Akaondoka Yerusalemu, akakutana nao katika nchi ya Hamathi, asiwape nafasi yoyote ya kuingia katika nchi yake.
26Akapeleka wapelelezi kambini mwao, wakarudi wakamwarifu ya kuwa wanajipanga, tayari kuwashambulia usiku.
27Jua lilipokuchwa, Yonathani aliwaagiza watu wake wawe macho, wameshika silaha zao usiku kucha ili wawe tayari kwa vita. Akaweka askari wa zamu kulizunguka kambi lake.
28Adui waliposikia kwamba Yonathani na watu wake wapo tayari kwa vita waliogopa na kutetemeka moyoni.
29Lakini Yonathani na watu wake hawakujua hayo, maana waliiona mioto ikiwaka.
30Yonathani akawafuatia asiwafikie, maana wamekwisha vuka mto Eleuthero.
31Basi, Yonathani akageuka, akashika njia nyingine, akawashambulia Waarabu waitwao Wazabidini, akawashinda na kuwateka nyara.
32Baada ya hayo, akaondoka akaenda Dameski akiipitia nchi yote.
33Simoni aliondoka, akashika njia kwenda Ashkeloni na ngome za karibu. Akageukia upande akaitwaa Yafa,
34maana alisikia ya kuwa watu wake walitaka kuitia mikononi mwa watu wa Demetrio. Akaweka kikosi cha askari kuilinda.
35Yonathani akarudi, akawaita wazee wa watu, akashauriana nao juu ya kujenga maboma katika Uyahudi,
36kuongeza kimo cha kuta za Yerusalemu, na kufanya boma refu kati ya ngome na mji ili kuitenga na mji, ikae peke yake, isiwepo nafasi ya kuuza na kununua.
37Walipokusanyika ili kujenga, sehemu ya ukuta kando ya kijito upande wa mashariki ilianguka, akatengeneza ule uitwao Kafenatha.
38Simoni naye alijenga Adida katika uwanda wa chini, akaifanya imara, akiweka milango na mapingo.
39Trifoni akataka kumiliki Asia na kuivaa taji, na kunyosha mkono wake juu ya mfalme Antioko.
40Alidhani ya kuwa Yonathani atamzuia hata labda kupigana naye; kwa hiyo alitafuta njia ya kumkamata na kumwua. Basi, akaondoka akaenda Beth-sheani.
41Yonathani akatoka na watu elfu arobaini hodari wa vita, kwenda kukutana naye, akafika Beth-sheani.
42Trifoni alipoliona jeshi lake kubwa aliogopa kumnyoshea mkono wake.
43Bali alimpokea kwa heshima, akamjulisha kwa rafiki wake wote, akampa zawadi. Akawaagiza rafiki zake na askari wake wamtii kana kwamba ni yeye mwenyewe.
44Akamwuliza Yonathani, Mbona umewachosha watu hawa wote, madhali hakuna vita kati yetu?
45Haya, basi, wape ruhusa waende zao. Chagua watu wachache wakae nawe, mfuatane nami hata Tolemaisi, nami nitaikabidhi kwako pamoja na ngome nyingine na askari wake na wakuu wao. Kisha nitageuka na kuondoka, maana ndiyo sababu ya kuja kwangu hapa.
46Akamsadiki, akafanya alivyosema, akawapa askari wake ruhusa, wakarudi Uyahudi.
47Akabaki na watu elfu tatu; katika hao aliacha wapatao elfu mbili Galilaya, akaenda na elfu moja.
48Lakini mara Yonathani alipoingia Tolemaisi, watu wa Tolemaisi waliifunga milango wakamkamata, na wote waliokuja naye waliwaua kwa upanga.
49Trifoni akapeleka askari na wapanda farasi waende Galilaya kwenye uwanda mkubwa kuwaua watu wote wa Yonathani.
50Na hao walipofahamu ya kuwa amekamatwa na kuuawa pamoja na watu wake walitiana moyo, wakajipanga kiaskari tayari kwa vita, wakaenda zao.
51Wale waliokuwa wakiwafuata walipoona ya kuwa wako tayari kujipigania waligeuka wakarudi nyuma.
52Wote wakafika nchi ya Uyahudi salama, wakamwombolezea Yonathani na watu wake, na kuogopa sana; Israeli yote ikafanya kilio kikubwa.
53Mataifa waliowazunguka walikusudia kuwaharibu kabisa, maana walisema, Hawana kiongozi wala msaidizi, basi tupigane nao sasa na kulifuta kumbukumbu lao katika wanadamu.