2 Wafalme 5

2 Wafalme 5

Kuponywa kwa Naamani

1Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake BWANA alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma.[#1 Fal 8:41-43; Lk 4:27; Kut 11:3; 2 Fal 4:8; Est 9:4]

2Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani.

3Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.

4Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi.

5Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi.[#1 Sam 9:8; 2 Fal 8:8,9]

6Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake.

7Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami.[#Mwa 37:29; 30:2; 1 Sam 2:6; Kum 32:39]

8Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.[#Kut 4:30]

9Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha.

10Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Nenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi.[#2 Fal 4:41; Yn 9:7]

11Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nilidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la BWANA, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma.[#1 Kor 2:14]

12Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira.[#Mit 14:17; 16:32; Mhu 7:9; Efe 4:31; Kol 3:8; Yak 1:19]

13Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?

14Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.[#Ayu 33:25; Lk 4:27]

15Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na wote aliofuatana nao. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani kote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee zawadi kutoka mtumwa wako.[#Lk 17:15; 1 Sam 17:46,47; Isa 43:10,11; Yer 10:10,11; Rum 10:10; Dan 2:47; 3:29; Mwa 33:11]

16Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa.[#2 Fal 3:14; Mwa 14:23; Mt 10:8; Mdo 8:18,20]

17Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA.

18Jambo hili BWANA amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, BWANA amwachilie mtumwa wako jambo hili.[#2 Fal 7:2,17]

19Elisha akamwambia, Nenda kwa amani.

Choyo cha Gehazi

Lakini Naamani alipokuwa ameenda mbali kidogo,

20Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama BWANA aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake.[#Kut 20:17; Yos 6:18; 1 Sam 8:3-5; Zab 10:3; Mit 1:19; 15:27; Lk 12:15; Kol 3:5; 1 Tim 6:10]

21Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani?

22Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana wa manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili.

23Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamsihi, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakatangulia mbele yake wakiwa wameyabeba.

24Naye alipofika kilimani, alivichukua kutoka mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao.

25Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali.[#Mit 30:20; Eze 33:31; Mit 12:22; Mdo 5:3]

26Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi?[#Zab 63:11; 140:11; Mit 13:21; Isa 3:11; 57:21; Mdo 13:9]

27Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.[#1 Tim 6:10; Kut 4:6; Law 13:2,3; 14:3,35; Hes 12:10; 2 Fal 15:5; 2 Nya 26:19,20]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania