Ezra 5

Ezra 5

Ujenzi wa hekalu waanza tena

1Basi manabii, Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido, wakawafanyia unabii Wayahudi waliokuwako Yerusalemu na Yuda; waliwafanyia unabii kwa jina la Mungu wa Israeli.[#Hag 1:1; Zek 1:1]

2Ndipo akaondoka Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, wakaanza kuijenga nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na pamoja nao walikuwa manabii wa Mungu, wakiwasaidia.[#Hag 1:12-15; Ezr 6:14; Mhu 12:11; Hag 2:4-9]

3Wakati ule ule Tatenai, Mkuu wa mkoa wa ng'ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzao, wakawajia, wakawaambia, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu?[#Ezr 6:6]

4Ndipo wakawauliza hivi, Majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani?

5Lakini jicho la Mungu lilikuwa likiwaelekea wazee wa Wayahudi, hao wasiwazuie hadi habari ile imfikie Dario, ndipo jawabu litakapopatikana kwa waraka.[#2 Nya 16:9; Ezr 7:6,28; Zab 33:18; Isa 41:10; 1 Pet 3:12]

6Hii ndiyo nakala ya waraka ambao; Tatenai, Mkuu wa mkoa wa ng'ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzake wa Kiajemi, waliokuwako huko ng'ambo ya Mto; walimtumia mfalme Dario.[#Ezr 4:9]

7Walimtumia ripoti; na maneno haya yakaandikwa ndani yake;

Kwa Dario, mfalme Salamu sana.

8Na ajue mfalme ya kuwa sisi tuliingia nchi ya Yuda, tukafika kunako nyumba ya Mungu mkuu, iliyojengwa kwa mawe makubwa, na miti imetiwa katika kuta zake, na kazi hii inaendelea kwa bidii, na kusitawi katika mikono yao.

9Ndipo tukawauliza wale wazee, tukawaambia hivi, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu?

10Tukawauliza pia majina yao, ili kukuhakikishia, tupate kuandika majina ya watu waliokuwa wakubwa wao.

11Wakatujibu hivi, wakasema, Sisi tu watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunaijenga nyumba iliyojengwa zamani sana, yapata miaka mingi, ambayo mfalme mkuu wa Israeli aliijenga na kuimaliza.[#Yos 24:15; Zab 119:46; Yon 1:9; Mt 10:32; Lk 12:8; Mdo 27:23; 1 Fal 6:1]

12Lakini hapo baba zetu walipomkasirisha Mungu wa mbingu na nchi, hata akaghadhibika, akawatia katika mkono wa Nebukadneza, mfalme wa Babeli, Mkaldayo, naye ndiye aliyeiharibu nyumba hii, akawachukua watu mateka mpaka Babeli.[#2 Nya 34:24,25; 36:16,17; 2 Fal 24:2; Yer 39:1]

13Lakini katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Babeli, Koreshi, mfalme, alitoa amri ijengwe tena nyumba ya Mungu.[#Ezr 1:1]

14Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, alivyovitoa Nebukadneza katika hekalu lililokuwako Yerusalemu, na kuviingiza katika hekalu la Babeli, vyombo hivyo mfalme Koreshi alivitoa katika hekalu la Babeli, akakabidhiwa mtu, jina lake Sheshbaza, ambaye alikuwa amemfanya mtawala;[#Ezr 1:7,8; Hag 1:14]

15naye akamwambia, Chukua vyombo hivi, uende, ukavitie katika hekalu lililoko Yerusalemu, na nyumba ya Mungu na ijengwe mahali pake.

16Ndipo yule Sheshbaza alipokuja, akaupiga msingi wa nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na tangu wakati ule hadi leo imekuwa ikijengwa, wala bado haijamalizika.[#Ezr 3:8,10; 6:15]

17Basi, sasa, mfalme akiona vema, watu na wachunguze katika nyumba ya hazina ya mfalme, iliyoko huko Babeli, kama ni kweli ya kuwa mfalme Koreshi alitoa amri kuijenga nyumba hiyo ya Mungu katika Yerusalemu, na mfalme akatutumie habari ya mapenzi yake kuhusu jambo hili.[#Ezr 6:1,2; Mit 25:2]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania