Yudithi 3

Yudithi 3

Kutaka amani

1Wakampelekea wajumbe na maneno ya amani, wakisema,

2Tazama, sisi watumwa wa Nebukadreza mfalme mkuu, tupo mbele yako; ufanye nasi kama inavyokupendeza.

3Tazama, makao yetu na ardhi yetu yote, na mashamba yetu ya ngano, na ng'ombe zetu na kondoo zetu, na mazizi yote ya mahema yetu, yako mbele yako; uyatumie kama inavyopendeza machoni pako

4Tazama, hata miji yetu ni yako, nao wanaoikaa; uje iufanyie kama unavyoona vema.

5Wale watu wakamwendea Holofene wakamwambia hayo yote sawasawa na maneno hayo.

6Basi, akaishukia nchi ya pwani, yeye na jeshi lake, akaweka vikosi vya askari katika miji mikubwa, akachukua watu kadha wa kadha katika miji hiyo wafuatane naye.

7Wakampokea kwa taji za maua na ngoma na matari, wao na watu wa nchi zote za jirani.

8Akaiharibu miji yao yote, na kuvikata vichaka vya msitu, maana aliamriwa kuiharibu miungu yote ya nchi makusudi mataifa yote wamwabudu Nebukadreza tu, na watu wa lugha zote na kabila zote wamwite mungu wao.[#Kut 34:13; 2 Nya 17:6]

9Akaenda Esdreloni karibu na Dotea, kando ya milima mikubwa ya Yuda. Akapiga kambi kati ya Geba na Beth-sheani, akakaa huko mwezi mzima ili apate kuvikusanya vyombo vyote vya jeshi lake.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania