The chat will start when you send the first message.
1Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.[#Yn 1:1,3; Ebr 1:10; Ayu 38:4; Isa 44:24; Rum 1:20; Kol 1:16; Ebr 11:3; Ufu 4:11]
2Nayo nchi ilikuwa tupu, tena bila umbo, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.[#Yer 4:23; Isa 40:12]
3Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.[#2 Kor 4:6; Zab 33:9]
4Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza.
5Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya kwanza.[#Zab 74:16]
6Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.[#Ayu 37:18; Zab 33:6; 136:5; Yer 10:12; 2 Pet 3:5]
7Mungu akaliumba anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.
8Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.
9Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo.[#Ayu 26:10; 38:8; Zab 33:7; 95:5]
10Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
11Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mimea itoayo mbegu, na miti ya matunda izaayo matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo.[#Ebr 6:7; Lk 6:44]
12Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
13Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.
14Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili ya kuonesha majira, siku na miaka;[#Kum 4:19; Ayu 25:3,5; Zab 74:16; 136:7]
15tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo.
16Mungu akaumba mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.
17Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi[#Zab 8:1]
18na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
19Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne.
20Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na viumbe vyenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu.[#Zab 104:24]
21Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
22Mungu akavibariki, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi.
23Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano.
24Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.[#Zab 104:18-23]
25Mungu akaumba aina zote za wanyama wa porini na wa kufugwa na viumbe vyote vitambaavyo juu ya nchi; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
26Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi.[#Zab 100:3; Efe 4:24; Yak 3:9; Zab 8:6]
27Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.[#1 Kor 11:7; Efe 4:24; Kol 3:10; Mal 2:15; Mt 19:4; Mk 10:6; Mwa 5:1-2]
28Mungu akawabariki, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuimiliki; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.[#Zab 127:3; 1 Tim 4:3; Mwa 9:1,7; Law 26:9; Zab 128:3,4]
29Mungu akasema, Tazama, nimewapa ninyi kila mmea utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndiyo chakula;[#Ayu 36:31; Zab 104:14,15; 136:25; 146:7; Mdo 14:17]
30na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndio chakula chenu; ikawa hivyo.[#Zab 145:15,16; 147:9; Ayu 38:41]
31Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.[#Zab 104:24; 1 Tim 4:4]