Mika 3

Mika 3

Watawala na manabii waovu

1Nikasema, Tafadhali sikieni, enyi vichwa vya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli. Je! Haiwapasi ninyi kujua hukumu?[#Yer 5:4,5]

2Ninyi mnaoyachukia mema, na kuyapenda mabaya; ninyi mnaowachuna watu ngozi yao, na nyama mifupani mwao.

3Naam, mnakula nyama za watu wangu, na kuwachuna ngozi zao, na kuivunja mifupa yao; naam, kuwakata vipande vipande kama kwa kutiwa chunguni, na kama nyama sufuriani.[#Zab 14:4]

4Ndipo watakapomwomba BWANA, asiwaitikie; naam, atawaficha uso wake wakati huo, kwa kadiri walivyotenda mabaya kwa matendo yao.[#Mit 1:28]

5BWANA asema hivi kuhusu manabii wanaowakosesha watu wangu; hao waumao kwa meno yao, na kulia, Amani; na mtu awaye yote asiyetia kitu vinywani mwao, wao humwandalia vita.[#Isa 56:10; Mt 7:15]

6Kwa hiyo itakuwa usiku kwenu, msipate kuona maono; tena itakuwa giza kwenu, msiweze kubashiri; nalo jua litawachwea manabii, nao mchana utakuwa mweusi juu yao.[#Eze 13:23]

7Na hao waonaji wataaibika, na wenye kubashiri watafadhaika; naam, hao wote watajifunika midomo yao; kwa maana; hapana jawabu la Mungu.[#Zab 74:9; Amo 8:11]

8Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa Roho ya BWANA; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubirie Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake.[#1 Kor 2:1,4; Isa 58:1]

9Sikieni haya, tafadhali, enyi vichwa vya nyumba ya Yakobo, mnaoitawala nyumba ya Israeli, mnaochukia hukumu, na kuipotosha adili.

10Wanaoijenga Sayuni kwa damu, na Yerusalemu kwa uovu.

11Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea BWANA, na kusema, Je! Hayupo BWANA katikati yetu? Hapana neno baya lolote litakalotufikia.[#Isa 1:23; Eze 22:12; Hos 4:18; Mik 7:3; Yer 6:13; Tit 1:11; 1 Sam 4:5,6; Isa 48:2]

12Basi, kwa ajili yenu, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu; na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni.[#Mik 1:6; Zab 79:1; Yer 26:18]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania