Zaburi 14

Zaburi 14

Kushutumiwa kwa wasiomwamini Mungu

1Mpumbavu husema moyoni, Hakuna Mungu;[#Rum 3:10-12; Zab 10:4; Mit 1:7,22; Mwa 6:12]

Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo,

Hakuna atendaye mema.

2Toka mbinguni BWANA aliwachungulia wanadamu,

Aone kama yuko mtu mwenye hekima,

Amtafutaye Mungu.

3Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja,

Hakuna atendaye mema,

La! Hata mmoja.

4Je! Wote wafanyao maovu hawajui?

Walao watu wangu kama walavyo mkate,

Hawamwiti BWANA.

5Hapo ndipo waovu watakaposhikwa na hofu nyingi,

Maana Mungu yupo pamoja na kizazi cha haki.

6Mnaiharibu mipango ya mtu mnyonge,

Bali BWANA ndiye aliye kimbilio lake.

7Laiti wokovu wa Israeli ungetoka katika Sayuni!

BWANA awarudishapo wafungwa wa watu wake;

Yakobo atashangilia,

Israeli atafurahi.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania