Zaburi 142

Zaburi 142

Sala ya ukombozi kutoka kwa watesi

1Kwa sauti yangu nitamlilia BWANA,[#1 Sam 22:1; 24:3]

Kwa sauti yangu nitamwomba BWANA dua.

2Nitafunua mbele zake malalamiko yangu,

Shida yangu nitaitangaza mbele zake.

3Roho yangu inapozimia unayajua mapito yangu;

Katika njia niendayo wamenifichia mtego.

4Utazame mkono wangu wa kuume ukaone,

Kwa maana sina mtu anijuaye.

Makimbilio yamenipotea,

Hakuna wa kunitunza roho.

5BWANA, nimekuita nikasema, Ndiwe kimbilio langu,[#Omb 3:24]

Fungu langu katika nchi ya walio hai.

6Ukisikilize kilio changu,[#Zab 116:6; 7:1]

Kwa maana nimedhilika sana.

Uniponye kutoka kwao wanaonifuatia,

Kwa maana wao ni hodari kuliko mimi.

7Uitoe nafsi yangu kifungoni.[#Zab 34:2; 119:17]

Nipate kulishukuru jina lako.

Wenye haki watanizunguka,

Kwa kuwa Wewe unanikirimu.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania