Sira 10

Sira 10

1Mtawala mwenye busara huwaelimisha watu wake,

utawala wa mtu mwenye akili una utaratibu mzuri.

2Alivyo mtawala, ndivyo walivyo na maofisa wake;

alivyo mkuu ndivyo walivyo na wakazi wa nchi yake.

3Mfalme asiye na nidhamu ni maangamizi kwa watu wake;

fanaka ya mji yatokana na maarifa ya viongozi wake.

4Utawala wa dunia uko mikononi mwa Bwana,

yeye humweka mtawala afaaye kwa wakati wake.

5Ufanisi wa binadamu umo mikononi mwa Bwana.

Bwana ndiye ampaye heshima mwandishi.

Kiburi

6Usichukizwe na kila kosa la jirani yako,

wala usifanye chochote kwa mkikimkiki wa ghadhabu.

7Kiburi huchukiwa na Mungu na binadamu;

udhalimu ni jambo la kuchukiza kwa wote wawili.

8Kwa sababu ya udhalimu, kiburi na kupenda utajiri,

mamlaka ya taifa moja huchukuliwa na taifa lingine.

9Je, mtu aliye vumbi na majivu atajivunia nini?

Hata alipo hai matumbo yake yananuka.

10Ugonjwa wa muda mrefu humduwaza daktari,[#10:10 Mstari huu katika makala za Kiebrania na Kigiriki si dhahiri.]

leo ni mfalme kesho ni maiti.

11Maana yanayowapata wote katika kifo ni sawa:

Wadudu, wanyama wakali na minyoo.

12Mwanzo wa kiburi ni kumwacha Bwana

na kuupindua moyo wake mbali na muumbaji wake.

13Maana chanzo cha kiburi ni dhambi

na mtu anayeambatana nacho atabubujika uchafu.

Ndiyo maana Bwana huwaletea adhabu wasiyoitazamia

watu wa namna hiyo na kuwaangamiza kabisa.

14Bwana amewaondoa wakuu kwenye viti vyao vya enzi,

na mahali pao amewaketisha wanyenyekevu.

15Bwana amewangoa wenye kiburi na mizizi yao,

na mahali pao amewaweka wanyenyekevu.

16Bwana amezifuta nchi za mataifa duniani,

na huyaangamiza hadi kwenye misingi ya dunia.

17Mataifa mengine ameyaondoa na kuyaangamiza,

na kufuta kumbukumbu lao duniani.

18Kiburi hakikuumbwa kwa ajili ya watu,

wala ghadhabu kwa ajili ya binadamu.

Watu wa kuheshimiwa

19Viumbe gani vinavyostahili heshima? Binadamu.

Viumbe gani vinavyostahili heshima? Wale wamchao Bwana.

Viumbe gani visivyostahili heshima? Binadamu.

Viumbe gani visivyostahili heshima? Wanaovunja amri.

20Kati ya ndugu mkubwa wao anastahili heshima.

Wanaomcha Mungu hustahili heshima mbele yake. [

21Kumcha Mungu ni mwanzo wa mafanikio;

lakini ukaidi na kiburi ni mwanzo wa kutofanikiwa.]

22Matajiri, waheshimiwa na maskini,

wajivunie kumcha Bwana.

23Si vema kumdharau mtu aliye maskini lakini ana akili,

wala si vizuri kumheshimu mwenye dhambi.

24Mtawala, hakimu na mwenye cheo ni wa kuheshimiwa,

lakini anayemcha Mungu ni mkuu kuliko hao wote.

25Mtumwa mwenye hekima atahudumiwa na watu huru;

na mwenye busara hatanungunika juu yake.

Kujishusha na kujiheshimu

26Usijioneshe kuwa mtaalamu ufanyapo kazi yako,

wala usijisifu wakati una taabu.

27Afadhali mtu mwenye bidii kazini na ana kila kitu,

kuliko mtu anayezurura akijigamba na hana chakula.

28Mwanangu, jisifu kwa unyenyekevu,

na ujione wewe mwenyewe ustahilivyo.

29Mtu anayejipatiliza mwenyewe nani atamwona hana hatia?

Nani atakayemheshimu mtu anayejidharau mwenyewe?

30Maskini huweza kuheshimiwa kwa maarifa yake;

na tajiri kwa utajiri alio nao.

31Anayeheshimiwa akiwa maskini

bila shaka ataheshimiwa zaidi akiwa tajiri!

Anayedharauliwa akiwa tajiri

bila shaka atadharauliwa zaidi akiwa maskini!

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania