Sira 16

Sira 16

Mungu atawaadhibu wenye dhambi

1Usitamani kuwa na watoto wengi wasio na faida;

wala kujivunia watoto wa kiume wasiomcha Mungu.

2Wakiongezeka usifurahi kwa sababu yao,

isipokuwa kama wanamcha Bwana.

3Usiwe na imani juu ya kuendelea kwao kuishi;

usitegemee wingi wao.

Maana, mtoto mmoja ni bora kuliko elfu;

ni afadhali kufa bila mtoto,

kuliko kuwa na watoto wasiomcha Mungu.

4Mji utajaa watu kwa busara ya mtu mmoja,

lakini kwa kabila moja la wabaya utabaki mtupu.

5Macho yangu yameona mambo mengi kama haya;

masikio yangu yamesikia mambo ya ajabu kuliko hayo.

6Moto utawashwa katika kusanyiko la wenye dhambi,

ghadhabu iliwashwa katika taifa lililoasi.

7Yale majitu ya zamani hakuyasamehe,

majitu ambayo kwa kutegemea nguvu zao yaliasi.

8Mungu hakuwahurumia jirani za Loti,

watu ambao alichukizwa na kiburi chao.

9Hakulionea huruma taifa lililopangiwa kuangamizwa,

taifa lililofutiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zake;

10hata wale wanajeshi 600,000 wa miguu

ambao walikusanyika pamoja, wakaasi kwa kiburi chao.

11Hata kama kuna mtu mmoja mwenye kiburi,

itakuwa ajabu kama hataadhibiwa.

Maana Bwana ni mwenye huruma na ghadhabu.

Yeye ana nguvu kuu ya kusamehe na huwaka hasira;

na wale wasiotubu anawamwagia ghadhabu yake.

12Kama zilivyo kuu huruma zake ndivyo na karipio lake.

Yeye humhukumu mtu kulingana na matendo yake.

13Mwenye dhambi hataweza kutoroka na alichonyakua;

na tazamio la wanaomcha Mungu halitakuwa bure.

14Mwadilifu atapokea anayostahili,

kila mtu atapokea kulingana na matendo yake. [

15Bwana alimfanya Farao awe na kiburi hata asimkiri Bwana; ili ulimwengu ujue kazi za Bwana.

16Huruma yake ni wazi kwa viumbe vyote; alitenga kati ya mwanga wake na giza kwa kamba ya kupimia.]

17Usiseme, “Nitajificha mbali na Bwana;

na hamna yeyote huko juu atakayenikumbuka!

Kati ya watu wengi hivyo sitajulikana,

maana, nafsi yangu ni kitu gani kati ya viumbe visivyohesabika?”

18Tazama, mbingu na mbingu za juu kabisa,

kuzimu na dunia, vyote vitatetemeka,

wakati Bwana atakapokuja.

19Milima na misingi ya dunia hutetemeka,

wakati Bwana anapoviangalia.

20Lakini hakuna binadamu anayefikiri hayo;

ni nani awezaye kuelewa njia za Mungu?

21Usiseme: “Nikitenda dhambi hakuna anionaye.

Nikitenda hayo katika siri kuu nani atajua?

22Na nikitenda mema nani atayataja?

Nani anangojea apewe taarifa?

Yeye hukawia mno kutekeleza agano lake.”

23Ndivyo afikiriavyo mtu asiye na akili;

mtu mjinga aliyepotoshwa hufikiri kipumbavu.

Hekima ya Mungu katika maumbile

24Mwanangu, nisikilize ujifunze maarifa.

Tega sikio usikie maneno yangu.

25Nitakupa mafunzo mazitomazito,

nitakufundisha maarifa kwa usahihi.

26Mungu alipoumba kazi zake mwanzoni[#16:26 Kiebrania kazi … mwanzoni: Kigiriki: Katika hukumu ya Bwana, kazi zake ni tangu mwanzo.]

alizifanya ziwepo na kuzipa mpango,

27akazipa mpango wa kufuata milele,

tangu mwanzo wake na vizazi vyote.

Hivyo hazitindikiwi wala kuchoka

na haziachi kutekeleza wajibu wao.

28Hakuna hata mojawapo inayosongana na nyingine

na wala haziachi kutii neno lake Mungu.

29Baada ya hayo yote Bwana aliiangalia dunia

akaijaza vitu vyake vizuri.

30Aliifunika dunia kwa kila aina ya viumbe,

ambavyo vitakufa na kurudi udongoni.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania