Sira 44

Sira 44

Sifa kwa wazee

1Sasa, na tuwasifu watu mashuhuri,

wazee wetu na vizazi vilivyopita.

2Bwana aliwapa fahari kubwa,

akawafanya wakuu tangu siku za kale.

3Walikuwako wale waliotawala falme zao,

watu mashuhuri kwa nguvu zao;

washauri waliojaa busara,

watangazaji wa unabii.

4Wengine waliongoza mataifa kwa mawazo yao,

wakawa wenye maarifa ya elimu kwa faida ya watu,

wenye hekima katika maneno na mafundisho yao.

5Walitunga nyimbo kwa ufundi,

wakabuni mashairi na kuyaandika.

6Walikuwa matajiri wenye mali tele,

waliishi kwa utulivu katika makazi yao.

7Hao wote waliheshimika katika vizazi vyao,

wakawa wenye fahari nyakati zao.

8Baadhi yao waliacha jina jema duniani,

na watu wakatangaza sifa zao mpaka leo.

9Wako na wengine ambao hawakumbukwi,

ambao wametoweka wakawa kama hawakuishi.

Walikuwa kana kwamba hawakupata kuzaliwa,

kadhalika na watoto wao baada yao.

10Lakini wale wengine walikuwa watu wema,

ambao matendo yao adili hayajasahaulika.

11Mali yao hubaki na wazawa wao,

na huo ndio urithi wao.

12Wazawa wao huzingatia agano,

na kwa ajili yao wataendelea kufanya hivyo.

13Nasaba yao itadumu milele,

na fahari yao haitafutika.

14Miili yao ilizikwa kwa amani,

na majina yao yanadumu kizazi hata kizazi.

15Watu watasimulia hekima yao,

na jumuiya ya watu itatangaza sifa zao.

Henoki na Noa

16Henoki alimpendeza Bwana, akachukuliwa mbinguni.

Yeye alikuwa mfano bora wa toba vizazi vyote.

17Noa alionekana mkamilifu na mwadilifu;

yalipokuja maangamizi, akawa mwanzo mpya wa binadamu.

Maana kwake watu waliachwa duniani, tufani ilipokuja.

18Bwana alifanya naye agano la milele,

kwamba viumbe vyote wasifutiliwe mbali kwa ile tufani.

Abrahamu, Isaka na Yakobo

19Abrahamu alikuwa mzee maarufu wa mataifa mengi,

hakuna aliyekuwa na fahari kama yeye.

20Alishika sheria ya Mungu Mkuu,

na Bwana akafanya agano naye,

akakamilisha katika mwili wake alama ya agano hilo,

naye Abrahamu alipojaribiwa, akaonekana kuwa mwaminifu.

21Hivyo Bwana akamhakikishia kwa kiapo

kwamba mataifa yatabarikiwa kwa njia ya wazawa wake;

kwamba wazawa wake watakuwa wengi kama mavumbi ya nchi.

Kwamba watakuwa wengi kama nyota,

na urithi wao tangu bahari hadi bahari,

tangu mto Eufrate mpaka miisho ya dunia.

22Vilevile Bwana alimpa Isaka uthibitisho ule ule

kwa ajili ya Abrahamu, baba yake.

Baraka za watu wote na agano lake,

23aliziweka juu ya Yakobo.

Alimwimarisha Yakobo kwa baraka zake,

akampa ile nchi iwe yake mwenyewe,

na kuigawa miongoni mwa makabila kumi na mawili.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania