Sira 51

Sira 51

Utenzi wa shukrani

1Nakushukuru, ee Bwana na Mfalme,

nakusifu, ee Mungu, Mwokozi wangu.

Nalitukuza jina lako.

2Maana wewe umekuwa mlinzi na msaidizi wangu.

Umeukomboa mwili wangu kutoka kwenye maangamizi,

kutoka kwenye mitego ya watu wadanganyifu,

na kutoka kwa watu wasemao uongo.

Mbele ya maadui zangu ulikuwa upande wangu;

umekuwa msaada wangu, umenikomboa.

3Kwa ukuu wa huruma yako na jina lako,

umenikomboa makuchani mwa maadui waliotaka kuniangamiza,

kutoka kwa wale waliotafuta maisha yangu,

kutoka katika mateso mengi niliyoyavumilia;

4kutoka katika moto ulionisonga pande zote,

moto ambao mimi sikuuwasha;

5kutoka katika vilindi vya kuzimu,

kutoka kwa wanaosema machafu na uongo,

na kutoka masengenyo ya ulimi mwovu.

6Nilikuwa kwenye nimekaribia kabisa kifo,

na maisha yangu yalikuwa karibu na chini kuzimu.

7Nilikuwa nimezungukwa kabisa,

sikuwa na yeyote wa kunisaidia.

Nilitazama nipate msaada wa binadamu,

lakini hakuna aliyenisaidia.

8Kisha nikakumbuka huruma zako, ee Bwana,

na kazi zako za tangu zamani,

kwamba wewe wawakomboa wale wanaokutegemea,

na huwaokoa makuchani mwa maadui zao.

9Nami nikapeleka juu kwako ombi langu,

nikakuomba uniokoe kutoka kwenye kifo.

10Namlilia Bwana: “Wewe u Baba yangu!

Usiniache katika siku ya mateso,

ambapo hakutakuwa na msaada dhidi ya adui.

11Nitalisifu jina lako daima,

nitakuimbia nyimbo za sifa na shukrani.”

Ombi langu lilipokelewa,

12maana uliniokoa nisiangamie,

ukanisalimisha wakati mbaya.

Kwa hiyo nitakushukuru na kukusifu,

nitalisifu jina la Bwana.

Shairi la kumtafuta Hekima

13Nilipokuwa bado mdogo, kabla sijaanza kusafiri,

kwa sala yangu nilitafuta hadharani nimpate Hekima.

14Nikiwa nimesimama nje ya hekalu nilimtafuta,

nami nitamtafuta mpaka mwisho.

15Tangu kuchanua kwake mpaka kuiva,

nilimfurahia sana moyoni mwangu.

Nyayo zangu zilifuata njia nyofu;

tangu ujana wangu nimezifuata njia zake.

16Nilitega sikio langu kidogo nikampokea Hekima,

nami nikajipatia mafunzo mengi.

17Nilizidi kuendelea kwa hekima,

naye atakayenipa hekima nitamtukuza.

18Maana niliamua kuishi kulingana na hekima,

nikawa na hamu sana ya kutenda mema,

na wala sitaaibishwa kamwe.

19Nilijishughulisha sana nipate hekima,

nikawa mwangalifu sana kuhusu mwenendo wangu.

Nilinyosha mikono yangu mbinguni kuomba,

nikalalamika kwa vile sikumjua Hekima.

20Niliielekeza nafsi yangu kwa Hekima,

nami nikampata kwa kujitakasa.

Kutoka kwake nilipata maarifa tangu mwanzo,

nami najua kwamba sitaachwa bila msaada wake.

21Moyo wangu ulipania kumtafuta Hekima,

ndiyo maana sasa nimepata utajiri mkubwa.

22Bwana alitunukia zawadi ya kuwa na ulimi,

nami nitautumia kumsifu yeye.

23Njoni kwangu enyi msiojua kitu,

ingieni na kukaa shuleni kwangu.

24Kwa nini mnalalamika kuwa hamna mambo haya,

na kwa nini mioyo yenu inaona kiu?

25Nilifungua kinywa changu na kusema:

“Jipatieni hekima bila kununua.”

26Inamisheni shingo zenu chini ya nira yake,

na kuacha mioyo yenu ipate mafunzo;

Hekima anapatikana karibu sana.

27Oneni wenyewe kwamba nimefanya kazi kidogo,

lakini nimejipatia amani kubwa.

28Jipatieni mafundisho kwa fedha nyingi,

nanyi mtajipatia nayo dhahabu nyingi.

29Mioyo yenu na ifurahie huruma ya Bwana,

wala msiaibishwe kamwe wakati mnapomsifu.

30Fanyeni kazi yenu kabla ya wakati uliopangwa,

naye Mungu awapeni tuzo lenu wakati wake!

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania