The chat will start when you send the first message.
1Usifanye uovu, na uovu wowote hautakupata.
2Epa ubaya, nao utakukimbia.
3Mwanangu, usilime ardhi kupanda udhalimu,
la sivyo utavuna udhalimu mara saba.
4Usiombe cheo kikubwa kwa Bwana,
wala kiti cha heshima kwa mfalme.
5Usijioneshe kuwa mwadilifu mbele ya Bwana,
wala usioneshe hekima yako mbele ya mfalme.
6Usijaribu kutafuta kuwa hakimu,
usije ukashindwa kutokomeza uovu;
usije ukapotoshwa na mwenye nguvu,
na hivyo kusababisha kupoteza unyofu wako.
7Usiiudhi jumuiya ya wananchi,
wala usijivunjie heshima miongoni mwa watu.
8Usivutwe kutenda dhambi mara mbili,
maana hutaacha kuadhibiwa hata kwa mmoja.
9Usiseme, “Mungu atapokea wingi wa sadaka zangu;
nikimtolea Mungu Mkuu tambiko lazima atapokea.”
10Usisitesite katika sala,
wala usisahau kuwapa maskini sadaka.
11Usimcheke aliye na huzuni rohoni,
maana Mungu anayemnyenyekeza mtu aweza pia kumwinua.
12Usitunge uongo dhidi ya ndugu yako,
wala usimtendee hivyo rafiki yako.
13Kataa kabisa kusema uongo,
maana uongo hauleti jema lolote.
14Usipayukepayuke kwenye mkutano wa wazee,
wala kujirudiarudia katika sala zako.
15Usichukie kazi ngumu,
au kazi ya shambani iliyopangwa na Mungu Mkuu.
16Usijiunge na genge la wenye dhambi,
kumbuka kuwa adhabu haitakawia.
17Uwe mnyenyekevu kabisa,
maana adhabu ya wasiomcha Mungu ni moto na mabuu.
18Usimsaliti rafiki ili kujipatia fedha,
au rafiki wa kweli kujipatia dhahabu ya Ofiri.
19Uoe mwanamke mwenye hekima na mwema;
mwanamke mwema ni bora kuliko dhahabu.
20Usimtendee vibaya mtumishi mwaminifu kazini,
au kibarua aliyejitolea kukutumikia vema.
21Mpende mtumwa mwenye akili kwa moyo wote;
usimnyime mtumwa wa namna hiyo uhuru wake.
22Je, una mifugo? Basi, ichunge!
Kama ina faida kwako, baki nayo.
23Je, una watoto? Basi, wafunze nidhamu.
Wafundishe utii tangu utoto wao.
24Je, una watoto wa kike?
Wafunze usafi wa mwili,
lakini usiwabembeleze mno.
25Ukimwoza binti yako utakuwa umetimiza kazi kubwa.
Lakini mwoze kwa mwanamume mwenye busara.
26Unaye mke anayekupendeza? Usimpe talaka.
Lakini kama humpendi, usimwamini.
27Mheshimu baba yako kwa moyo wako wote,
wala usisahau uchungu wa mama yako alipokuzaa.
28Kumbuka kwamba wao ndio waliokuzaa.
Je, unaweza kuwalipa yote waliyokutendea?
29Mche Bwana kwa moyo wako wote;
na wape heshima makuhani wake.
30Mpende Muumba wako kwa nguvu zako zote,
na usiwatupe wahudumu wake.
31Mche Bwana na kuwaheshimu makuhani.
Mpe Bwana sehemu ulivyoamriwa:
Mazao ya kwanza, tambiko ya hatia,
kidari, na zaka zote zinazotakiwa.
32Wape maskini kwa ukarimu,
ili Bwana akupe baraka zake kikamilifu.
33Ukarimu wako uwe kwa watu wote,
wala usiwanyime ukarimu hata marehemu.
34Usiwape kisogo wanaoomboleza,
bali ushiriki huzuni ya walio na huzuni.
35Usiache kuwatembelea wagonjwa;
maana ukiwatembelea utapendwa.
36Katika matendo yako yote kumbuka mwisho wako,
nawe hutatenda dhambi kamwe.