Hekima ya Solomoni 12

Hekima ya Solomoni 12

1Roho yako isiyokufa imo katika vitu vyote.

2Kwa hiyo wawakosoa kwa taratibu wale wanaokukosea;

na kuwakumbusha na kuwaonya juu ya yale wanayokukosea nayo,

ili waachane na ubaya wao na kukutumainia wewe, ee Bwana.

Ubaya wa watu wa Kanaani

3Pia wale wakazi wa awali wa nchi yako takatifu,

4uliwachukia kwa sababu walifanya mambo ya kuchukiza mno:

Walifanya uchawi na ibada chafu;

5walichinja watoto bila huruma,

wakala nyama na damu za watu kama sadaka;

walishiriki ibada za siri,

6na mauaji ya watoto wasioweza kujitetea.

Kwa kupenda kwako watu hao waliangamizwa na wazee wetu,

7kusudi nchi hiyo unayoithamini kuliko zote

iwe makao ya watu wanaofaa kuwa watumishi wako.

8Lakini hata hawa uliwaonea huruma maana ni watu tu.

Ulipeleka nyuki watangulie jeshi lako

ili kuwaangamiza polepole.

9Ungaliweza kuwaruhusu watu wema wawaangamize waovu vitani;

au ungaliweza kuwaangamiza kwa wanyama wakali au kwa neno moja kali.

10Lakini ulitekeleza hukumu yako polepole kuwapa fursa ya kutubu;

ingawa ulijua kwamba kwa asili walikuwa waovu:

Walikuwa wakorofi tangu kuzaliwa kwao

na kwamba hawangeweza kubadili mawazo yao.

11Naam, wao walikuwa wamelaaniwa tangu awali,

wala si kwa kumwogopa mtu yeyote ndipo ukawaacha kuwaadhibu kwa dhambi zao.

Mungu ana uwezo juu ya yote

12Nani awezaye kukuuliza kisa cha matendo yako,

au kupinga uamuzi wako?

Nani atakushtaki kwamba umeangamiza mataifa uliyoyaumba?

Nani awezaye kuja mbele yako kuwatetea watu hao waovu?

13Hakuna mungu mwingine ila wewe

ambaye huyaangalia maslahi ya wote

nawe wapaswa kutambuliwa kwamba umehukumu kwa haki.

14Wala hakuna mfalme au mtawala yeyote awezaye kukushtaki

ukiwa umemwadhibu mtu yeyote.

15Kwa vile wewe ni mwadilifu na watawala kwa uadilifu

kamwe hutumii nguvu yako kumwadhibu asiyestahili adhabu.

16Uwezo wako ni asili ya uadilifu;

wawaonea huruma watu wote kwa maana wewe ni Bwana wa wote.

17Iwapo binadamu hasadiki kwamba uwezo wako ni mkamilifu,

basi, wewe huidhihirisha nguvu yako,

na kuwafadhaisha wale wanaojua uwezo wako lakini hawaujali.

18Ingawa unao uwezo mkuu, hata hivyo wahukumu kwa upole;

na watutawala kwa uvumilivu mkubwa

maana unao uwezo wa kuadhibu wakati wowote upendao.

19Kwa matendo yako umewafundisha watu wako

kwamba mtu aliye mwadilifu anapaswa kuwa mpole.

Umewapa watoto wako matumaini makubwa,

maana watu wakikosa unawajalia uwezekano wa kutubu.

20Wewe ulikuwa mwangalifu na mwenye uvumilivu

katika kuwaadhibu maadui za watu wako ingawa walistahili kufa;

uliwapa fursa kubwa ya kuachana na uovu wao.

21Lakini watu wako wewe mwenyewe uliwahukumu vikali,

ingawa ulikuwa umewaapia na kuwaahidia wazee wao mambo mema.

22Basi, watuadhibu sisi,

lakini wawaadhibu maadui zetu mara elfu kumi zaidi

kusudi wakati tunapohukumu tuukumbuke wema wako

na wakati tunapohukumiwa tutazamie kupata huruma.

Adhabu ya Wamisri

23Basi, wale walioishi vibaya na kipumbavu,

uliwatesa kwa vitu vyao vya kuchukiza.

24Walipotea mbali katika makosa,

wakaabudu vinyama ambavyo hata maadui zao walividharau;

walidanganyika kama watoto wapumbavu.

25Hivyo kama watoto wasio na akili,

uliwaletea adhabu wakazomewa.

26Lakini wale wanaodharau kuonywa kwa adhabu kidogo,

watauona uzito wa adhabu Mungu atakayowapa.

27Walipoadhibiwa kwa viumbe vilevile walivyodhani kuwa miungu,

walipumbazika wakafahamu kwamba Mungu wa kweli ni yuleyule waliyekuwa wanakataa kumtambua.

Kwa hiyo walipata adhabu kali kabisa.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania