The chat will start when you send the first message.
1Naam, hukumu zako ni kuu mno na ngumu kueleza;
ndiyo maana wasiotaka kufunzwa hupotea.
2Maana watu wakorofi walipodhani wamelitia taifa lako chini ya nguvu zao,
wao wenyewe walifungwa katika usiku mrefu wa giza,
wamefungiwa nyumbani mwao mbali na uangalizi wako wa daima.
3Walidhani kwamba dhambi zao zilikuwa siri na zisizofichuliwa,
zikikingwa zisionekane kwa pazia jeusi la usahaulifu;
lakini sasa walikumbwa na hofu ya kutisha,
wakafadhaika na kutawanyika kwa kuona mizimu.
4Hata nyumba zao za giza walimokaa hazikuwakinga na hofu.
Walizungukwa na sauti za kutisha;
mizimu yenye huzuni na nyuso za kukunjamana iliwatokea.
5Hakuna moto uliokuwa na nguvu ya kuwaangazia,
wala nyota angavu hazikuweza kulimulika lile giza la kifo.
6Walitokewa tu na moto wa ajabu usiowashwa na binadamu ukawaangazia,
na kwa hofu yao wakaamini kwamba hayo waliyoyaona yalikuwa ya kutisha
kuliko walivyotazamia kuona.
7Hila walizofanya kwa uchawi wao zilishindwa
na hekima yote waliyojisifia ikaaibishwa.
8Maana wale waliodai watafukuza hofu na fadhaa kutoka kwa mgonjwa,
wao wenyewe walikuwa sasa wagonjwa kwa woga wa kuchekesha.
9Hata wakati hapakuwa na kitu cha kutisha,
wao walikumbwa na hofu kwa sauti za nyoka na vinyama vilivyotambaa.
10Waliangamia kwa kutetemeka kwa woga,
wakikataa hata kuiangalia hewani jambo lisiloepukika!
11Uovu msingi wake ni woga, na unajipatiliza wenyewe.
Mwenye dhamiri yenye hatia anaona daima mabaya kuliko ilivyo kweli.
12Woga ni ukosefu wa msaada ambao huletwa na akili timamu.
13Mtu anapokosa tumaini la ndani moyoni,
hujiachia kupatwa na hofu inayosababishwa na ujinga.
14Lakini wao, wakati wa usiku huo usiopumzisha
usiku unaotoka kwenye kutisha kuzimu,
wakiwa wanalala usingizi huo huo,
15pengine walifukuzwa kwa vivuli vya kutisha
au walikufa ganzi na kulegea rohoni mwao;
woga wa ghafla usiotazamiwa uliwakumba.
16Hivyo mtu yeyote aliyekuwa humo alizimia,
akawa amefungwa katika gereza lisilo na fito za chuma.
17Wakulima, wachungaji,
au vibarua waliofanya kazi porini,
wote walipatwa na vituko hivyo visivyoepukika,
maana wote walifungwa kwa mnyororo ule ule wa giza.
18Kila waliposikia mvumo mdogo wa upepo,
au sauti tamu ya ndege katika matawi yaliyotanda,
au maporomoko ya maji yaendayo kasi,
19au mianguko ya miamba iliyovurumishwa,
au wanyama wasioonekana wakikimbia na kuruka,
au sauti za wanyama wakinguruma kwa ukali,
au hata miangwi katika mapango ya milima,
wao walizirai kwa hofu.
20Ulimwengu wote ulimulikwa na nuru angavu,
na watu walishughulikia mambo yao bila wasiwasi;
21ni wao tu peke yao waliofunikwa kwa usiku huo mzito,
mfano wa giza lile la kifo lililokuwa linawangojea;
lakini wakawa mzigo mzito kwao wenyewe kuliko hata lile giza.