Hekima ya Solomoni 5

Hekima ya Solomoni 5

1Siku hiyo, mtu mwema atasimama kwa ujasiri mwingi,

mbele yao hao waliokuwa wanamtesa

na wale ambao walipuuza kazi zake.

2Watakapomwona watatetemeka kwa hofu kubwa,

watashangaa ameokolewaje bila wao kutazamia.

3Ndipo watakapojuta na kusemezana wao kwa wao

na kwa kuugua moyoni wataambiana:

4“Huyu ndiye mtu yuleyule tuliyemdhihaki zamani,

tukamwona ni kichekesho;

kweli tulikuwa wapumbavu.

Tulidhani aliishi kama mwendawazimu,

na alipokufa hatukumpa heshima.

5Imekuwaje sasa yuko pamoja na watoto wa Mungu

na anayo sehemu yake kati ya watakatifu wake!

6Kumbe sisi ndio tuliokiuka njia ya kweli!

Hatukuishi katika mwanga wa haki,

wala mwanga wake haukutuangaza.

7Sisi tulijaa upotovu na uharibifu;

tulitangatanga jangwani pasipo njia,

wala hatukujua njia ya Bwana.

8Kujigamba kwetu kumetufaa nini?

Tumepata faida gani kwa utajiri tuliojivunia?

9Vitu hivyo vyote vimepita kama kivuli;

naam, kama minongono inayotoweka.

10Ni kama meli ipasuayo mawimbi baharini,

lakini ikisha pita alama yake haionekani,

wala mkondo wake katika mawimbi.

11Au kama vile ndege arukavyo angani:

Haachi alama yoyote ya njia yake;

huipigapiga hewa nyepesi kwa mabawa yake,

huipenya kwa nguvu za kuruka kwake,

na huipasua kwa mapigo ya mabawa yake,

lakini haachi alama yoyote ya kupita kwake.

12Kadhalika mshale: Unapofyatuliwa kulenga shabaha,

hupenya hewa, lakini hewa hufumba mara moja;

wala hakuna mtu awezaye kutambua ulipopitia.

13Kadhalika nasi, mara baada ya kuzaliwa twatoweka,

bila hata kuacha nyuma alama yoyote ya wema,

bali tuliangamia katika uovu wetu wenyewe.”

14Matumaini ya mwovu ni kama makapi yapeperushwayo na upepo;

ni kama povu linalochukuliwa na tufani;

hutawanywa kama moshi mbele ya upepo,

hupita kama kumbukumbu ya mgeni wa siku moja.

15Lakini watu wema huishi milele

na tuzo lao liko kwa Bwana;

naam, Mungu Mkuu huwatunza.

16Kwa hiyo watapokea taji tukufu,

na kilemba maridadi mkononi mwa Bwana,

maana kwa mkono wake wa kulia atawafunika,

kwa mkono wake atawakinga kama kwa ngao.

17Atautwaa upendo wake mkuu kama zana za vita;

atavipa silaha viumbe vyote kufukuza maadui zake.

18Haki itakuwa kama vazi la kujikinga kifua,

hukumu ya haki itakuwa kama kofia yake ya chuma;

19utakatifu utakuwa ndio ngao yake imara.

20Atainoa ghadhabu yake kali kuwa upanga,

na ulimwengu wote utajiunga naye

kupigana na maadui wasio na akili.

21Umeme utaruka moja kwa moja na kupiga shabaha,

kama mishale kutoka uta imara mawinguni.

22Mvua ya mawe itawalenga kama kwa uta na mshale;

maji ya bahari yatafurika kwa hasira dhidi yao,

na mito itawaangamiza bila huruma.

23Upepo mkali utazuka dhidi yao,

na kuwapeperushia mbali kama kimbunga.

Upotovu utasababisha maangamizi nchini kote;

matendo maovu yataporomosha mamlaka ya watawala.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania