Danieli 3

Wenzake Danieli wanaokolewa motoni.

1Mfalme Nebukadinesari akatengeneza kinyago cha dhahabu, urefu wake ni mikono 60, nao upana wake ni mikono 6, akakisimamisha katika bonde la Dura katika nchi ya Babeli.

2Kisha mfalme Nebukadinesari akatuma wajumbe, awakusanye wenye amri na wakuu na watawala nchi na waamuzi na watunza mali na mabwana shauri na wandewa na wakuu wote wa nchi, waje kukieua kinyago hicho, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha.

3Ndipo, walipokusanyika wenye amri na wakuu na watawala nchi na waamuzi na watunza mali na mabwana shauri na wandewa na wakuu wote wa nchi kukieua kinyago hicho, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha, wakasimama mbele ya hicho kinyago, Nebukadinesari alichokisimamisha.

4Mpiga mbiu akatangaza kwa sauti ya nguvu kwamba: Ninyi makabila nanyi koo za watu walio wenye ndimi za watu mnaagizwa hivi:

5siku, mtakapozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za mazomari na za namna zote za ngoma, sharti mwanguke kukisujudia kinyago cha dhahabu, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha.

6Kila mtu atakayekataa kuanguka na kukisujudia atatupwa papo hapo ndani ya tanuru iwakayo moto.

7Kwa sababu hii siku ile ilipofika, wao wote wa makabila ya watu walipozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za namna zote za ngoma, basi, ndipo, makabila na koo zote za watu, wao wote wenye ndimi za watu walipoanguka wakikisujudia hicho kinyago cha dhahabu, mfalme Nebukadinesari alichokisimamisha.

8Kwa sababu hiyo siku zile wakaja waume wa Kikasidi wakawachongea Wayuda,

9wakamwambia mfalme Nebukadinesari hivyo: E mfalme, na uwe mwenye uzima kale na kale!

10Wewe mfalme umetoa amri kwamba: Kila mtu atakapozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za mazomari na za namna zote za ngoma sharti aanguke na kukisujudia hicho kinyago cha dhahabu.[#Dan. 6:12.]

11Kila mtu atakayekataa kuanguka na kukisujudia atatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto.

12Basi, wako waume wa Kiyuda, uliowaagizia kazi ya kuiangalia nchi ya Babeli, ndio Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego; waume hao hawakuishika amri yako, mfalme, wala hawaitumikii miungu yako, wala hawakiangukii hicho kinyago cha dhahabu, ulichokisimamisha.[#Dan. 2:49.]

13Ndipo, Nebukadinesari alipokasirika na kuchafuka sana, akaagiza kuwaleta akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, kisha waume hawa wakapelekwa kwake mfalme.

14Nebukadinesari akawauliza kwamba: Ninyi Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, mnakataaje kuitumikia miungu yangu na kukiangukia hicho kinyago cha dhahabu, nilichokiweka?

15Kama ninyi mko tayari siku, mtakapozisikia sauti za mabaragumu na za filimbi na za marimba na za mapango na za mazeze na za namna zote za ngoma, mwanguke na kukisujudia kila kinyago cha dhahabu, nilichokitengeneza, basi; lakini msipokiangukia, mtatupwa papo hapo ndani ya tanuru iwakayo moto. Tena yuko Mungu gani atakayewaokoa mkononi mwangu?[#2 Fal. 18:35.]

16Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego wakajibu, wakamwambia mfalme: Nebukadinesari, kwetu sisi ni kazi bure kukujibu neno moja tu.

17Tazama, Mungu wetu, tunayemtumikia sisi, ndiye anayeweza kutuokoa katika tanuru iwakayo moto, namo mkononi mwako, mfalme, atatuokoa.[#Sh. 66:12.]

18Lakini ijapo hataki kutuokoa, uvijue, wewe mfalme: miungu yako sisi hatutaitumikia, wala kinyago cha dhahabu, ulichokisimamisha, hatutakiangukia.[#2 Mose 20:3-5.]

19Ndipo, makali yenye moto yalipoushika moyo wote wa Nebukadinesari, nao uso wake ukawa mwingine kwa kuwaona akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, akaagiza kabisa kuwasha moto mkubwa katika tanuru kuupita moto wake wa siku zote mara saba.

20Kisha akaagiza watu walio wenye nguvu zaidi katika vikosi vyake, wawafunge akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, kisha wawatupe katika tanuru iwakayo moto.

21Kwa hiyo watu hawa wakafungwa pamoja na fulana zao na kanzu zao na shati zao na mavazi yao mengine, wakatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto.

22Kwa kuwa amri ya mfalme ilikuwa imetolewa kwa nguvu kabisa, ule ukali wa moto uliowaka sana ukawaua hao watu waliowachukua akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego.

23Lakini wale waume watatu, Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, wakaanguka ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamefungwa.

24Kisha mfalme Nebukadinesari akastuka, akainuka kwa upesi, akawaambia wasemaji wake wa shaurini kwamba: Je? Hatukutupa watu watatu ndani ya tanuru, nao walikuwa wamefungwa? Wakajibu, wakamwambia mfalme: Ndivyo kweli, mfalme.

25Akajibu akisema: Tena inakuwaje? Mimi ninaona watu wanne wasiofungwa kabisa, wanatembea motoni, tena hawaungui hata kidogo; naye wa nne sura yake anafanana na mwana wa Mungu.[#Dan. 3:28; Yes. 43:2.]

26Kisha Nebukadinesari akalikaribia lango la tanuru iwakayo moto, akaita kwamba: Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego mnaomtumikia Mungu Alioko huko juu, tokeni nje! Ndipo, Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego walipotoka motoni.

27Wenye amri na wakuu na watawala nchi na wasemaji wa shaurini wa mfalme waliokuwa wamekusanyika hapo wakaona, ya kuwa moto haukuweza kuwafanyizia kitu watu hawa, nywele za vichwani pao hazikuungua, wala nguo zao hazikugeuka kuwa nyingine, wala mnuko tu wa moto haukuwapata.[#Ebr. 11:34.]

28Nekukadinesari akasema kwamba: Na atukuzwe Mungu wao Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego, kwa kuwa amemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtegemea wakikataa kuifuata amri ya mfalme, wakaitoa miili yao, kwamba wasiangukie mungu wo wote na kuusujudia, ila Mungu wao tu.[#Dan. 6:22.]

29Kwa hiyo sasa inatoka amri kwangu kwamba: Kwao makabila na koo zote, kwao wote wenye ndimi za watu, kila atakayesema neno la kumkosea Mungu wao Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego atakatwa vipandevipande, nayo nyumba yake itageuzwa kuwa kifusi, kwa kuwa hakuna Mungu mwingine anayeweza kuponya hivyo.[#Dan. 2:47.]

30Ndipo, mfalme alipowaongezea akina Sadiraki na Mesaki na Abedi-Nego macheo yao ya kuliangalia jimbo la Babeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania