Mpiga mbiu 3

Mpiga mbiu 3

Matendo ya mtu hukoma, matendo yake Mungu hukaa.

1Kila jambo lina saa yake, kila jambo lipendezalo chini ya mbingu lina wakati wake:[#Mbiu. 8:6.]

2Kuzaliwa kuna wakati wake, nako kufa kuna wakati wake; kupanda kuna wakati wake, nako kuyang'oa yaliyopandwa kuna wakati wake.

3Kuua kuna wakati wake, nako kuponya kuna wakati wake; kubomoa kuna wakati wake, nako kujenga kuna wakati wake.

4Kulia kuna wakati wake, nako kucheka kuna wakati wake; kuomboleza kua wakati wake, nako kucheza kuna wakati wake.

5Kutupa mawe kuna wakati wake, nako kukusanya mawe kuna wakati wake; kukumbatiana kuna wakati wake, nako kukataa kukumbatiana kuna wakati wake.

6Kutafuta kuna wakati wake, nako kupoteza kuna wakati wake; kuweka kuna wakati wake, nako kutupa kuna wakati wake.

7Kurarua kuna wakati wake, nako kushona kuna wakati wake; kunyamaza kimya kuna wakati wake, nako kusema kuna wakati wake.

8Kupendana kuna wakati wake, nako kuchukiana kuna wakati wake; kupigana kuna wakati wake, nako kutengemana kuna wakati wake.

9Afanyaye kazi analo pato gani kwa kusumbuka kwake?

10Nikautazama utumishi, Mungu aliowapa wana wa Adamu kuutumikia.

11Yote aliyafanya kuwa mazuri wakati wao, akawapa kuziwaza mioyoni mwao nazo siku zijazo; ni hiyo tu, asiyowapa: mtu asiione maana ya kazi, Mungu aliyoifanya toka mwanzo hata mwisho.[#Mbiu. 8:17.]

12Ndipo, nilipojua, ya kuwa hakuna lililo jema kwao kuliko kufurahi na kufanya mema siku zao za kuwapo.

13Haya nayo nikayajua, ya kuwa kwake kila mtu apataye kula na kunywa na kuona mema kwa masumbuko yake, hiki nacho ni kipaji cha Mungu.

14Nikajua, ya kuwa yote, Mungu ayafanyayo, hukaa kale na kale; hapo hapana kuongeza wala kupunguza, kwani Mungu aliyafanya kuwa hivyo, watu wamwogope.

15Yaliyoko yalikuwako kale, nayo yatakaokuwako yalikuwako kale. Naye Mungu huyazusha yaliyopitishwa.

Kumcha Mungu kunatosha.

16Tena niliona, ya kuwa chini ya jua uko upotovu penye mashauri yanyokayo, napo penye wongofu uko upotovu.

17Ndipo, niliposema moyoni mwangu: Mungu atamhukumu mwongofu pamoja na mpotovu, kwani kila jambo lipendezalo aliliwekea wakati wake, hata matendo yote.[#Mbiu. 12:14.]

18Nikasema moyoni mwangu; Ni kwa ajili ya wana wa Adamu, Mungu akitaka kuwajaribu, waone, ya kuwa wao na nyama ni sawa.

19Kwani jambo la mwisho linalowapata wana wa Adamu nalo jambo la mwisho linalowapata nyama ni jambo lilo hilo moja; kama huyu anavyokufa, ndivyo, yule naye anavyokufa, pumzi yao wote ni moja tu. Kwa hiyo haliko, mtu analompita nyama, kwani yote ni ya bure.[#Sh. 49:13,20.]

20Wote pia hupaendea mahali pale pamoja: wote walitoka uvumbini, tena wote hurudi uvumbini.[#1 Mose 3:19.]

21Yuko nani ajuaye, kama roho za wana wa Adamu hupaa juu? au kama roho za nyama hushuka chini kuzimuni?[#Mbiu. 12:7.]

22Ndivyo, nilivyoona, ya kuwa hakuna mema, mtu ayapatayo kuliko kuzifurahia kazi zake, kwani hili ndilo fungu lake yeye. Kwani yuko nani atakayempeleka mahali, atakapoyaona.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania