The chat will start when you send the first message.
1Samusoni alipotelemka kwenda Timuna akaona huko Timuna mwanamke kwao vijana wa kike wa Wafilisti.
2Alipopanda kwao akamwambia baba yake na mama yake kwamba: Nimeona mwanamke huko Timuna kwao vijana wa kike wa Wafilisti, sasa mchukueni, awe mke wangu!
3Baba yake na mama yake wakamwambia: Kumbe kwetu hakuna mwanamke kwao vijana wa kike wa ndugu zako walio ukoo wetu, wewe ukienda kuchukua mwanamke kwao Wafilisti wasiotahiriwa? Lakini Samusoni akamwambia baba yake: Huyo mchukue, awe mke wangu! Kwani ndiye apendezaye machoni pangu.[#2 Mose 34:16.]
4Lakini baba yake na mama yake hawakujua, ya kuwa shauri hili limetoka kwa Bwana, ya kuwa yeye alitafuta njia ya kuwajia Wafilisti, maana wakati huo Wafilisti waliwatawala Waisiraeli.
5Samusoni alipotelemka kwenda Timuna pamoja na baba yake na mama yake, hapo, walipofika kwenye mizabibu ya Timuna, mara mwana wa simba akamkingia njiani na kumngurumia.
6Mara roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, akamrarua, kama ni kurarua mwana mbuzi, lakini hakuwa na mata mkononi mwake. Lakini baba yake na mama yake hakuwasimulia, aliyoyafanya.[#Amu. 13:25.]
7Kisha akaenda Timuna kuongea na yule mwanamke, naye akapendeza zaidi machoni pake Samusoni.
8Siku zilipopita, akarudi kumchukua. Alipotoka njiani, aende kuutazama ule mzoga wa yule simba, akaona, nyuki wengi wa porini wamo ndani ya mzoga wa simba, hata asali imo.
9Akaitwaa mikononi mwake, akaendelea njiani akiila. Kisha akaenda kwao baba yake na mama yake, akawapa nao, nao wakaila, lakini hakuwaambia, ya kuwa asali hii ameitwaa katika mzoga wa simba.
10Baba yake alipotelemka kwenda kwa yule mwanamke, Samusoni akafanya huko karamu, kwani ndivyo, vijana walivyofanya.
11Ikawa, walipomwona wakachukua wenzake 30 wa kuwa naye.
12Samusoni akawaambia: Na niwategee kitendawili! Kama mtaniambia maana yake siku hizi saba za karamu kwa kuitambua maana, basi, nitawapa ninyi kanzu 30 na mavazi mengine 30.
13Lakini msipoweza kuniambia maana yake, ninyi mtanipa kanzu 30 na mavazi mengine 30. Wakamwambia: Kitege kitendawili chako, tukisikie!
14Akawaambia:
Kwa mlaji kikatoka chakula, kwa mwenye nguvu kikatoka kitamu. Siku tatu hawakuweza kumwambia maana ya hicho kitendawili.
15Ikawa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samusoni: Mnyege mumeo, atuambie hicho kitendawili, tusikuchome moto pamoja na nyumba ya baba yako! Je? Mmetualika kuja huku, mpate kuzichukua mali zetu! Au sivyo?
16Ndipo, mkewe Samusoni alipomlilia na kumwambia: Kumbe unachukizwa na mimi, hunipendi! Wana wao walio ukoo wangu umewategea kitendawili, lakini mimi hujaniambia. Akamwambia: Tazama, hata baba yangu na mama yangu sikuwaambia, wewe nitawezaje kukuambia?
17Alipomlilia hizo siku saba za karamu yao, basi, siku ya saba akamwambia maana, kwani alimsumbua sana, naye akawaambia hicho kitendawili wale wana wa ukoo wake.[#Amu. 16:16-17.]
18Kwa hiyo watu wa ule mji wakamwambia siku ya saba, jua lilipokuwa halijachwa bado:
Kiko kitamu kuliko asali? Yuko mwenye nguvu kuliko simba?
Naye akawaambia:
Kama hamngalimtumia ndama wangu, hapo mlipolima, hicho kitendawili changu hamngaliona maana.
19Kisha roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, akatelemka kwenda Askaloni, akaua huko watu 30, akachukua yote, waliyokuwa nayo, nayo mavazi akawapa wao waliomwambia maana ya kitendawili, lakini makali yake yakawaka moto, aliporudi nyumbani mwa baba yake.
20Kisha mkewe Samusoni akawa mkewe mmoja wao wenzake, Samusoni aliyemchagua kuwa rafiki yake.[#Amu. 15:2.]