Yoeli 2

Yoeli 2

Nguvu za nzige.

1Pigeni baragumu Sioni!

Pigeni kelele milimani kwenye utakatifu wangu!

Wote wakaao katika nchi hii watetemeke,

kwa kuwa siku ya Bwana inakuja, iko karibu!

2Ni siku yenye giza lililozidi kabisa,

ni siku yenye mawingu yaliyo meusi;

kama wekundu wa kupambazuka unavyotandama milimani juu,

ndivyo, lile kabila linavyotokeza wengi walio wenye nguvu;

walio kama hao hawakuwako toka kale,

wala hawatakuwako tena nyuma yao

hata miaka ya vizazi na vizazi.

3Mbele yao moto unakula, nyuma yao miali ya moto inawaka;

mbele yao nchi ni kama bustani ya Edeni, nyuma yao ni jangwa tupu,

pasipatikane pa kuponea.

4Ukiwatazama, wanafanana kuwa kama farasi,

wanapiga mbio kama wapanda farasi.

5Uvumi wao ni kama wa magari yarukayo milimani juu

au kama uvumi wa moto ulao majani makavu;

ni kama wa watu wenye nguvu waliojipanga kupigana.

6Mbele yao watu wanajipinda, nyuso zao zikiwapoa.

7Wanapiga mbio kama wenye nguvu wa vitani,

wanakwea ukutani kama mafundi wa mapigano,

wanakwenda kila mmoja katika njia yake,

hawayapotoi kamwe mapito yao,

8wala hawasukumani wenyewe mtu na ndugu yake,

kila mmoja huendelea katika mkondo wake;

ingawa wengine wao waanguke kwa kupigwa, hawazuiliki.

9Wanaurukia mji wakizikwea kuta za bomani mbiombio,

wanapanda kuingia nyumbani na kujipenyeza madirishani

kama mwizi.

10Mbele yao nchi inatetemeka, nazo mbingu zinatikisika,

jua na mwezi unaguiwa na giza, nazo nyota zinakoma

kuangaza.

11Bwana anapiga ngurumo yake, ivitangulie vikosi vyake,

kwa kuwa kambi lake ni kubwa sana,

nao walitimizao neno lake ni wenye nguvu;

kwani siku ya Bwana ni kuu, inaogopesha sana,

yuko nani atakayeivumilia?

Kuwaita wote, wajute.

12Ndivyo, asemavyo Bwana:

Sasa hivi rudini kwangu kwa mioyo yenu yote

mkifunga kwa kulia na kuomboleza!

13Irarueni mioyo yenu, msiyararue mavazi yenu!

Kisha rudini kwa Bwana Mungu wenu!

Kwani Yeye ni mwenye utu na huruma,

tena mwenye uvumilivu na upole mwingi;

hugeuza moyo, asifanye mabaya.

14Labda atageuza moyo tena, atuachilie mbaraka

atakapoondoka,

akiwapatia vilaji na vinywaji vya kumtambikia Bwana mungu

wenu!

15Pigeni baragumu Sioni! Eueni mfungo! Utangazeni

mkutano!

16Wakusanyeni watu wa kwenu! Ueueni huo mkutano!

Waiteni wazee! Wakusanyeni nao wachanga, nao wanyonyao

maziwa!

Mchumba mume atoke chumbani mwake!

Naye mchumba mke atoke mwake, alimo!

17Watambikaji wanaomtumikia Bwana na walie

katikati ya ukumbi na meza ya kutambikia,

waseme: Bwana, wahurumie walio ukoo wako!

Usiwatoe walio fungu lako, watukanwe, wamizimu

wakiwatawala!

Mbona wataka, waseme kwa makabila mengine: Mungu wao yuko

wapi?

Kiagio cha mbaraka mpya.

18Ndipo, Bwana alipoionea nchi yake wivu,

akawahurumia walio ukoo wake.

19Bwana akajibu na kuwaambia walio ukoo wake:

Mtaniona, nikiwapatia ngano

na pombe mbichi na mafuta, myashibe!

Sitawatoa tena, mtukanwe na wamizimu.

20Nao wale waliotoka kaskazini

nitawaondoa kwenu, niwapeleke mbali,

niwakumbe, waende katika nchi kavu iliyo peke yake;

watangulizi wao nitawatupa katika bahari

iliyoko upande wa maawioni kwa jua,

wafuasi wao wa nyuma nitawatupa katika bahari

iliyoko upande wa machweoni kwa jua,

mnuko mbaya wa kuoza kwao utapanda juu,

kwa sababu watakuwa wamefanya makuu zaidi.

21Usiogope, wewe nchi! Ila shangilia kwa furaha!

Kwani Bwana atafanya jambo kuu.

22Msiogope, ninyi nyama wa porini!

Kwani mbuga za nyikani zitachipuka,

kwani miti itazaa matunda yao,

nayo mikuyu na mizabibu itatoa mazao ya nguvu.

23Wana wa Sioni, shangilieni! Mfurahieni Bwana Mungu wenu!

Kwani anawapa mvua ya masika hapo ipasapo,

anawanyeshea kwanza mvua za masika nazo za vuli.

24Ndipo, penye kupuria patakapojaa ngano,

nayo makamulio yatafurikiwa na mvinyo mbichi na mafuta.

25Nitawarudishia miaka

iliyoliwa nao nzige na funutu na bumundu na panzi,

ni vile vikosi vyangu vingi vyenye nguvu, nilivyovituma

kwenu.

26Mtakula kabisa na kushiba, mlisifu Jina la Bwana Mungu

wenu,

kwa kuwa alifanya kwenu mataajabu!

Kweli walio ukoo wangu hawatapatwa na soni kale na kale.

27Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi niko katikati ya

Waisiraeli,

ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wenu, siye mwingine.

Kweli walio ukoo wangu hawatapatwa na soni kale na kale.

Kiagio cha Roho Mtakatifu.

28Hayo yatakapokwisha, ndipo, itakapokuwa, niwamiminie Roho yangu wote walio wenye miili ya kimtu.

Nao wana wenu wa kiume na wa kike watasema na kufumbua;

nao wazee wenu wataoteshwa ndoto,

nao vijana wenu wataona maono.

29Nao walio watumwa wangu waume na wake

nitawamiminia Roho yangu siku zilezile.

30Nami nitafanya vioja mbinguni na nchini,

vyenye damu na moto na moshimoshi.

31Jua litageuka, liwe giza, nao mwezi utageuka, uwe damu

mbele ya kutimia kwake ile siku kubwa ya Bwana, inayoogopesha.

32Tena itakuwa, kila atakayelitambikia Jina la Bwana ataokoka.

Kwani mlimani pa Sioni namo Yerusalemu watakuwamo waliopona,

kama Bwana alivyosema;

namo miongoni mwao waliookolewa watakuwamo, Bwana aliowaita.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania