Yosua 2

Yosua 2

Wapelelezi wa Yeriko wanaponywa na mwanamke mgoni Rahabu.

1Yosua mwana wa Nuni, akatuma na kufichaficha toka Sitimu watu wawili kwenda kupeleleza, akiwaambia: Nendeni, mwitazame nchi hii nao mji wa Yeriko! Wakaenda, wakafikia nyumbani mwa mwanamke mgoni, jina lake Rahabu, wakalala huko.[#Yak. 2:25; Ebr. 11:31.]

2Mfalme wa Yeriko alipoambiwa: Tazama, wako watu waliotoka kwa wana wa Isiraeli, wamekuja usiku huu kuipeleleza nchi hii,

3mfalme wa Yeriko akatuma kwa Rahabu kumwambia: Watoe wale watu waliokuja kwako na kuingia nyumbani mwako, kwani wamekuja kuipeleleza nchi hii yote.

4Lakini yule mwanamke akawachukua wale watu wawili, akawaficha, kisha akasema: Kweli wale watu walifika kwangu, lakini sikujua, walikotoka.

5Tena hapo, malango yalipofungwa jioni, wale watu wakatoka, nami sikujua, wale watu walikokwenda. Wafuateni upesi kwa kupiga mbio, na mwakamate.

6Lakini alikuwa amewapandisha darini na kuwaficha katika makonge yaliyotandikwa naye huko darini.

7Nao wale watu wakawafuata upesi wakishika njia ya kwenda Yordani mpaka huko vivukoni. Hao waliowafuata upesi walipokwisha kutoka, wakalifunga lango la mji.

8Wale walipokuwa hawajalala bado, yule mwanamke akapanda darini na kufika huko, walikokuwa,

9akawaambia wale watu: Ninajua, ya kuwa Bwana amewapa nchi hii, asi tukaingiwa na mastuko kwa kuwaogopa ninyi, nao wenyeji wote wa nchi hii mioyo yao imeyeyuka kwa ajili yanu ninyi;[#2 Mose 23:27.]

10kwani tumesikia, jinsi Bwana alivyokausha mbele yenu maji ya Bahari Nyekundu, mlipotoka Misri, tena mliyowatendea wale wafalme wawili wa Waamori, Sihoni na Ogi, waliokuwako ng'ambo ya huko ya Yordani, mliowaangamiza kabisa kwa kuwatia mwiko wa kuwapo.[#2 Mose 14:21; 4 Mose 21:24,35.]

11Tulipoyasikia, mioyo yetu ikayeyuka, hakuna mtu asiyekatika roho kwa ajili yenu, kwani Bwana Mungu wenu ni Mungu huko mbinguni juu, hata huku chini katika nchi.[#Yos. 5:1; 2 Mose 15:14-15; 5 Mose 4:39.]

12Sasa niapieni na kumtaja Bwana kwamba: Kama mimi nilivyowatendea mema, ndivyo, nanyi mtakavyoutendea mema mlango wa baba yangu, mnipe kielekezo cha welekevu wenu,

13mkiacha kuwaua akina baba na mama na ndugu zangu wa kiume na wa kike nao wote wa kwao, mkiziponya roho zetu, tusife.

14Wale watu wakawaambia: Tutazitoa roho zetu, ziwakomboe ninyi kufani, msipoyaeleza haya mambo yetu. Hapo, Bwana atakapotupa nchi hii, tutakufanyizia mambo mema yenye welekevu.

15Kisha akawashusha kwa kamba dirishani, kwani nyumba yake ilikuwa imejengwa juu ya boma la mji; hapo juu ya boma ndipo, alipokaa.

16Akawaambia: Nendeni milimani kujificha huko siku tatu, wanaowafuata wasiwapate! Wao wanaowafuata watakaporudi, basi, mtakwenda zenu.

17Wale watu wakamwambia: Kwa ajili ya hicho kiapo, ulichotuapisha, hatutakora manza,

18ila itakuwa hivyo: sisi tutakapoingia katika nchi hii, sharti ulifunge kamba hili la nyuzi nyekundu hapa dirishani, ulipotushusha, kisha baba yako na mama yako na ndugu zako nao wote walio wa mlango wa baba yako uwakusanye kwako humu nyumbani.

19Na viwe hivyo: kila atakayetoka milangoni: pa nyumbani mwako kwenda nje, damu yake itamjia kichwani pake, lakini sisi tutakuwa hatumo; lakini kila atakayekuwa kwako humu nyumbani, damu yake itatujia sisi vichwani petu, kama mkono wa mtu utampiga.

20Tena mtakapoyaeleza hayo mambo yetu, sisi tutakuwa hatufungwi tena na hicho kiapo, ulichotuapisha.

21Akawaambia: Kama mlivyosema, basi, na viwe hivyo. Kisha akawaondokesha, wakaenda zao, naye akalifunga lile kamba jekundu dirishani.

22Walipokwenda, wakaenda milimani, wakakaa huko siku tatu, mpaka wao waliowafuata wakirudi; nao hao waliowafuata waliwatafuta njiani po pote, lakini hawakuwaona.

23Kisha wale watu wawili wakarudi wakishuka milimani na kuvuka mtoni; walipofika kwake Yosua, mwana wa Nuni, wakamsimulia yote yaliyowapata.

24Wakamwambia Yosua: Kweli Bwana ameitia hiyo nchi yote mikononi mwetu, nao wenyeji wote wa nchi hiyo wameyeyuka mioyo kwa ajili yetu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania