The chat will start when you send the first message.
1Mtu husema: Nimejisumbua, Mungu,
kweli nimejisumbua, Mungu, nikawezekana.
2Mimi ninapumbaa kama nyama,
utambuzi wa kimtu sinao.
3Sikujifunza werevu wa kweli, nimjue Mtakatifu,
kama wengine wanavyomjua.
4Ni nani aliyepaa mbinguni, ashuke chini?
Ni nani aukusanyaye upepo magaoni mwake?
Ni nani aliyeyafunga maji katika vazi lake?
Ni nani aliyeyashupaza mapeo yote ya nchi?
Jina lake ni nani? Tena jina la mwanawe ni nani?
Unayajua wewe?
5Kila neno la Mungu ni nguvu,
ni ngao yao wamkimbiliao.
6Maneno yake usiyaongeze kwa kutia jingine,
asije kukukanya, ukajulikana kuwa mwongo.
7Ninakuomba maneno haya mawili,
usininyime hayo, nikiwa ningaliko sijafa bado.
8Yaliyo upuzi na maneno ya uwongo yaweke mbali yasinifikie!
Usinipe kuwa mkosefu wa mali wala mwenye mali nyingi!
Ila nipe tu, nile chakula changu kinipasacho!
9Nisije kwa kushiba, nikabisha kwamba: Bwana ni nani?
Wala nisije kwa ukosefu, nikaiba, nikalikosea Jina la Mungu wangu.
10Usimsingizie mtumishi kwa bwana wake,
asikuapize, ukajipatia mapatilizo.
11Kiko kizazi cha watu wawaapizao baba zao,
wasiwabariki wamama zao.
12Kiko kizazi cha watu waliotakata machoni pao wenyewe,
nao hawakujiosha, uchafu wao uwatoke.
13Kiko kizazi cha watu walio wakuu zaidi machoni pao wenyewe,
nazo kope za macho yao huelekezwa juu sana.
14Kiko kizazi cha watu wenye panga kuwa meno yao,
wenye majisu kuwa magego yao,
hutaka kuwala wanyonge, watoweke katika nchi,
nao wakiwa, watoweke katika watu.
15Mruba ana wana wawili wa kike: Nipe! Nipe!
Viko vitu vitatu visivyoshiba, tena vinne visivyosema: Basi.
16Ni kuzimu na tumbo lisilozaa,
ni nchi isiyoshiba maji na moto usiosema: Basi.
17Jicho la mtu amfyozaye baba yake,
akakataa kumtii mama yake,
sharti kunguru waling'oe mtoni,
liliwe na makinda ya kozi.
18Yako mambo matatu, ninayoyastaajabu sana,
tena yako manne, nisiyoyajua maana:
19njia ya tai angani na njia ya nyoka mwambani
na njia ya merikebu baharini na njia ya mtu na mwanamwali.
20Ndivyo, njia ya mwanamke mgoni ilivyo:
hula, kisha hufuta kinywa chake na kusema: Sikukosa neno.
21Yako mambo matatu yanayoitetemesha nchi,
tena yako manne, nchi isiyoweza kuyavumilia:
22ni mtumwa akipata ufalme,
ni mpumbavu akishiba sana vyakula,
23ni mwanamke aliyechukizwa akiolewa,
ni mjakazi akizipata mali za bibi yake, ziwe fungu lake.
24Wako nyama wanne walio wadogo katika nchi kuliko wengine,
nao ni werevu walioerevuka kweli.
25Ni siafu: kweli hawana nguvu,
lakini huvitengneza vyakula vyao siku za mavuno yao.
26Ni pelele: wao si wenye nguvu,
lakini huweka nyumba zao magengeni.
27Ni nzige: hawana mfalme,
lakini hutoka wote pia vikosi kwa vikosi.
28Ni mijusi: mtu anaweza kuwakamata kwa mikono,
lakini namo majumbani mwa wafalme wamo.
29Wako watatu wenye mwendo upendezao,
tena wako wanne wenye mwendo mzuri.
30Ni simba awapitaye nyama wote nguvu,
harudi nyumba kwa kuona cho chote.
31Ni farasi mwenye matandiko kiunoni, ni beberu naye,
tena ni mfalme akiviongoza vikosi vyake.
32Kama umepumbaa kwa kujikuza, au kama umewaza mabaya moyoni,
kifumbe kinywa kwa kukibandikia mkono!
33Kwa kusukasuka maziwa huleta siagi,
tena kuzidi kukamua pua hutoa damu,
nako kuchochea makali huleta ugomvi.