1 Wamakabayo 2

1 Wamakabayo 2

MATATHIA ANAANZISHA VITA VITAKATIFU

Matathia na wanawe

1Siku zile Matathia, mwana wa Yohana, mwana wa Simeoni, kuhani wa ukoo wa Yoaribu, aliondoka Yerusalemu akakaa Modini.

2Alikuwa na wana watano: Yohana, aliyeitwa Gadi;

3Simoni, aliyeitwa Thasi;

4Yuda, aliyeitwa Makabayo;

5Eleazari, aliyeitwa Auarani; na Yonathani, aliyeitwa Afusi.

6Akayaona mambo ya kufuru yaliyotendeka katika Uyahudi na Yerusalemu,

7akasema, Ole wangu! Kwa nini nilizaliwa kuuona uharibifu wa watu wangu na maangamizo ya mji mtakatifu, hata kukaa kimya unapotiwa katika mikono ya adui zake, na patakatifu pake katika mikono ya wageni?

8Nyumba yake imekuwa kama ya mtu asiye na heshima,

9Vyombo vyake vya fahari vimetekwa na kuchukuliwa;

Watoto wake wameuawa njiani,

Na vijana wake kwa upanga wa adui!

10Taifa lipi lisiloyashiriki mateka yake?

Ufalme upi usioziteka mali zake?

11Mapambo yake yote yameondolewa,

Naye aliyekuwa muungwana amekuwa mtumwa!

12Naam, vyombo vitakatifu vyetu na fahari yetu

Na utukufu wetu vimefanywa ukiwa;

Vimetiwa unajisi na watu wa mataifa.

13Mbona, basi, tuzidi kuishi?

14Matathia na wanawe wakararua nguo zao, wakajivika magunia, wakalia kwa majonzi.

Kukataliwa kwa ibada ya mataifa

15Watumishi wa mfalme waliokuwa wakiwashurutisha watu kuasi wakaja Modini kuwalazimisha watu kutoa dhabihu.

16Waisraeli wengi wakatokea, hata Matathia na wanawe walikuwapo.

17Watumishi wa mfalme wakamwambia Matathia, Wewe u kiongozi, mtu mkuu, maarufu katika mji huu. Una wana wako na ndugu zako wa kujiweka upande wako.

18Basi, tangulia wewe, uitimize amri ya mfalme, kama walivyofanya watu wote wa mataifa, na watu wa Uyahudi, nao waliosalia Yerusalemu. Ndipo wewe na wana wako watahesabiwa kati ya rafiki za mfalme; naam, wewe na wana wako watatuzwa fedha na dhahabu na vipawa vingi.

19Matathia akajibu, akasema kwa sauti kuu. Hata mataifa yote katika milki ya mfalme wakimtii, akiacha kila mtu dini ya wazee wake na kuchagua kuzifuata amri za mfalme, lakini mimi sivyo.

20Mimi na wanangu na ndugu zangu tutaishika njia ya agano la baba zetu.

21Isiwe kwetu kujitenga na sheria na maagano, hasha!

22Sisi hatutaisikiliza amri ya mfalme tugeuke katika dini yetu, kwa kulia wala kwa kushoto.

23Alipokwisha kusema hayo, Myahudi mmoja alijitokeza machoni pa watu wote kusudi atoe dhabihu juu ya madhabahu iliyokuwapo Modeni, kama ilivyoamriwa na mfalme.

24Matathia alipomwona, alishikwa na ghadhabu, moyo wake ukatetemeka. Hasira yake ikatokeza hukumu, akamwendea mbio, akamwua pale madhabahuni.

25Kisha alimwua yule mtu wa mfalme naye, aliyekuwa akiishurutisha dhabihu, akaiangusha madhabahu.

26Hivyo alionesha juhudi yake kwa sheria, kama juhudi ya Finehasi juu ya Zimri, mwana wa Salu.[#Hes 25:6-15]

27Kisha, Matathia alipiga mbiu mjini kwa sauti kuu, akisema, Kila aliye na juhudi kwa ajili ya sheria na kutaka kulitetea agano, na anifuate!

28Naye na wana wake wakakimbilia milimani, wakiviacha vyote walivyokuwa navyo mjini.

Wayahudi washika Sabato jangwani na kuuawa

29Ndipo wengi waliokuwa wakitafuta haki na hukumu walikwenda jangwani wafanye maskani yao huko,

30pamoja na wana wao, wake zao na wanyama wao, kwa sababu ya maovu yaliyowalemea.

31Habari zikawafikia watumishi wa mfalme na askari waliokuwapo Yerusalemu, kwamba watu kadha wa kadha waliokuwa wameidharau amri ya mfalme wamekwenda kujificha jangwani.

32Wengi wao wakawafuatia wakawafikia, wakajipanga juu yao siku ya Sabato.[#2 Mak 6:11]

33Wakawaambia, Basi sasa! Tokeni, mfanye kama mfalme alivyoamuru, nanyi mtaishi.

34Wakasema, Hatutatoka, wala hatutaitii amri ya mfalme kuinajisi siku ya Sabato.

35Ndipo wakawashambulia.

36Nao hawakujilinda, wala kuwatupia jiwe, wala hata kuyaziba mashimo walimojificha.

37Maana walisema, Tufe wote katika usafi wetu, Mbingu na nchi zatushuhudia ya kuwa mnatuua bila haki.

38Wakawashambulia siku ya Sabato, wakafa, pamoja na wake zao na watoto wao na wanyama wao, watu wapatao elfu.

Kazi za Matathia na wafuasi wake

39Matathia na rafiki zake walipopata habari

40waliambiana, Kama sisi sote tutafanya kama walivyofanya ndugu zetu, tusipigane na watu wa mataifa kwa ajili ya nafsi zetu na amri zetu, watatufuta upesi katika nchi.

41Wakafanya shauri siku ile ya kuwa; Kama mtu yeyote akituletea vita siku ya Sabato, tupigane naye; tusife wote kama ndugu zetu waliokufa katika maficho yao.

Jibu la mashambulizi

42Wakati huo kundi la Wahasidimu walijiunga nao, Waisraeli hodari wa vita waliojitoa kwa hiari kuitetea sheria.

43Na wote walioyakimbia maovu walikuja kwao na kuwaongezea nguvu.

44Wakakusanya jeshi kubwa, wakawapiga wenye dhambi katika hasira yao, na walioasi katika ghadhabu yao; na waliobaki waliwakimbilia mataifa, wajisalimishe kwao.

45Matathia na rafiki zake wakazungukazunguka wakizivunja madhabahu za miungu,

46na kutahiri kwa shuruti watoto wote wasiotahiriwa waliowapata katika mipaka ya Israeli.

47Wakawafuatia wana wa uovu, na kazi ilifanikiwa mikononi mwao.

48Wakaiokoa sheria katika mikono ya mataifa na wafalme, wasikubali wenye dhambi wainue pembe zao.

Wasia wa Matathia

49Siku za kufa kwake Matathia zilipokaribia, aliwaambia wanawe: Siku hizi jeuri na lawama vimeongezeka nguvu; ndio wakati wa uharibifu na hasira kali.

50Basi wanangu, mwe na juhudi kwa sheria, mtoe maisha yenu kwa ajili ya agano la baba zenu.

51Yakumbukeni matendo ya baba zenu waliyoyatenda katika vizazi vyao, ili mpate utukufu na jina la milele.

52Je, Abrahamu hakuonekana kuwa amini alipojaribiwa, ikahesabika kwake kuwa haki?[#Mwa 15:16; 22:15-18]

53Yusufu, wakati wa kutaabika kwake, aliishika amri, naye akapata kuwa bwana wa Misri.[#Mwa 39:1—45:28]

54Finehasi, baba yetu, kwa sababu alikuwa na juhudi nyingi, alipewa ahadi ya ukuhani wa milele.

55Yoshua, kwa kulitimiza neno, alikuwa mwamuzi katika Israeli.[#Hes 13:1—14:12]

56Kalebu, kwa kutoa ushuhuda katika mkutano, alipata urithi katika nchi.

57Daudi, mwenye rehema, alikirithi kiti cha ufalme wa milele.[#2 Sam 7:16]

58Eliya, kwa kuwa aliona wivu mwingi kwa ajili ya sheria, alichukuliwa juu mbinguni.[#2 Fal 2:9-12]

59Hanania, Azaria na Mishaeli waliamini, wakaokolewa katika moto.[#Dan 6:1-24; DaJok 1:31-42]

60Danieli, kwa kuwa hakuwa na hatia, aliponywa vinywani mwa simba.[#Mwa 2:7; Mhu 3:20; 12:7]

61Fikirini, basi, vizazi kwa vizazi, hakuna wawekao imani kwake Yeye watakaokosa nguvu.

62Msiyaogope maneno ya mtu mwenye dhambi, maana fahari yake itakuwa samadi na funza.

63Leo atainuka, na kesho hataonekana kamwe, amerudia udongo wake na mawazo yake yamepotea.

64Basi, ninyi, wanangu, mwe hodari, simameni imara kwa ajili ya sheria, maana kwa hayo mtatukuzwa.

65Tazama, Simoni ndugu yenu, najua ya kuwa yu mtu wa shauri; msikilizeni sikuzote; atakuwa baba kwenu.

66Yuda Makabayo, shujaa tangu ujana wake, atakuwa jemadari wenu na kuwapigania watu wenu.

67Nanyi, wapokeeni wote wanaoishika sheria, mkatoze kisasi cha maovu waliyotendwa watu wenu.

68Wapatilizeni mataifa na kuyaangalia maneno ya sheria.

69Akawabariki, akakusanyika kwa baba zake.

70Alikufa katika mwaka wa mia moja arubaini na sita, akazikwa katika kaburi la baba zake huko Modeni. Israeli yote ikamfanyia maombolezo makuu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya