The chat will start when you send the first message.
1Ikawa siku zile hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao waende vitani, ili kupigana na Israeli. Naye Akishi akamwambia Daudi, Jua hakika ya kuwa wewe utatoka pamoja nami jeshini, wewe na watu wako.[#1 Sam 29:1]
2Naye Daudi akamwambia Akishi, Vema, sasa utajua atakayoyatenda mtumishi wako. Naye Akishi akamwambia Daudi, Haya basi! Mimi nitakufanya wewe kuwa mlinzi wangu binafsi daima.[#Rum 12:9]
3Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi.[#Law 19:31; 20:27; Kum 18:10-11; 1 Sam 25:1; Isa 57:1,2; Mdo 16:16,19; Kut 22:18]
4Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa.[#Yos 19:18; 2 Fal 4:8; 1 Sam 31:1]
5Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana.[#Ayu 15:21; 18:11; Zab 48:5,6; 73:19; Isa 57:20; Dan 5:6]
6Lakini Sauli alipouliza kwa BWANA, BWANA hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii.[#Hes 27:21; 1 Sam 14:37; Mit 1:28; Omb 2:9; Hes 12:6; Kut 28:30; Kum 33:8]
7Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori.
8Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye pamoja na watu wawili wakamfikia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukaniletee yeye nitakayemtaja kwako.[#Kum 18:11; 1 Nya 10:13; Isa 8:19]
9Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua?
10Naye Sauli akamwapia kwa BWANA, akasema, Aishivyo BWANA, haitakupata adhabu yoyote kwa jambo hili.
11Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekuletea? Naye akasema, Niletee Samweli.
12Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli.[#Isa 57:2; Ufu 14:13]
13Mfalme akamwambia Usiogope; unaona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu akitoka katika nchi.[#Kut 22:28; Zab 138:1]
14Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka chini, akasujudia.[#1 Sam 15:27; 2 The 2:10,11]
15Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje.[#Mit 5:11; 14:14; 1 Sam 18:12]
16Samweli akasema, Kwa nini unaniuliza mimi, wakati BWANA amekuacha, naye amekuwa adui yako?
17Yeye BWANA amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; BWANA amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi.[#1 Sam 15:28]
18Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya BWANA, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii BWANA amekutendea hili leo.[#1 Sam 15:3-9; 1 Fal 20:42; 1 Nya 10:13; Yer 48:10]
19Tena pamoja na wewe BWANA atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena BWANA atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti.
20Mara Sauli akaanguka chini kifudifudi, akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli, wala hakuwa na nguvu yoyote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha.[#1 Sam 25:37; Ayu 15:20-24; Zab 50:21]
21Ndipo yule mwanamke akamwendea Sauli na alipoona kuwa yeye ametaabika sana, akamwambia, Angalia, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako, nami nimehatarisha uhai wangu, nami nimeyasikiliza maneno yako uliyoniambia.[#Amu 12:3; 1 Sam 19:5; Ayu 13:14]
22Basi sasa, tafadhali, wewe uisikilize sauti ya mjakazi wako, nikakuandalie angaa mkate kidogo; ukale, ili upate nguvu, utakapokwenda zako.
23Lakini yeye alikataa, akasema, Mimi sitaki kula. Ila watumishi wake, pamoja na yule mwanamke, wakamlazimisha; naye akaisikiliza sauti yao. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.[#Mwa 4:6; 1 Fal 21:4; Mit 25:20,21]
24Naye yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona nyumbani; akafanya haraka kumchinja; akatwaa na unga, akaukanda, akafanya mkate wa mofa kwa unga huo;[#Mwa 18:7,8; Lk 15:23-30]
25kisha akamwandalia Sauli na watumishi wake; wakala. Ndipo wakaondoka, wakaenda zao usiku ule.