The chat will start when you send the first message.
1Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu),[#Gal 1:11,12]
2na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia;
3Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo;[#Rum 1:7]
4ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.[#Gal 2:20; 1 Tim 2:6; Tit 3:14; 1 Yoh 5:19]
5Utukufu una yeye milele na milele, Amina.
6Nashangaa kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia Injili ya namna nyingine.
7Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza Injili ya Kristo.[#Mdo 15:1,24]
8Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiria ninyi Injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiria, na alaaniwe.[#1 Kor 16:22]
9Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiria ninyi Injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.
10Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.[#1 The 2:4]
11Kwa maana, ndugu zangu, Injili hiyo niliyowahubiria, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu.
12Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.
13Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba nililitesa kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu.[#Mdo 8:3; 22:4-5; 26:9-11]
14Nami niliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu.[#Mdo 22:3]
15Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,[#Mdo 9:3-6; 22:6-10; 26:13-18; #Rum 1:1; Yer 1:5; Isa 49:1]
16alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubirie Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu;[#Gal 2:7; Mt 16:17]
17wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nilikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski.
18Kisha, baada ya miaka mitatu, nilipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano.[#Mdo 9:26-30]
19Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana.[#Mt 13:55]
20Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo.
21Baadaye nilikwenda pande za Shamu na Kilikia.[#Mdo 9:30]
22Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Yudea yaliyokuwa katika Kristo;
23ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetutesa hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani.
24Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.