The chat will start when you send the first message.
1Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ni bwana wa yote;
2bali yuko chini ya mawakili na watunzaji, hadi wakati uliokwisha kuamriwa na baba.
3Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.[#Gal 3:23; 5:1; Kol 2:20; #4:3 Katika Kigiriki ni ‘Kawaida za kwanza za dunia’.]
4Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,[#Efe 1:10]
5kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.[#Rum 8:15-17; #Gal 3:13,26]
6Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.[#Rum 8:15]
7Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.[#Gal 3:29; Rum 8:16,17]
8Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu.
9Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena?
10Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka.[#Rum 14:5; Kol 2:16]
11Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.[#2 Yoh 1:8]
12Ndugu zangu, nawasihi, iweni kama mimi, maana mimi ni kama ninyi. Hamkunidhulumu kwa lolote.[#2 Kor 2:5]
13Lakini mwajua ya kuwa niliwahubiria Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili;[#Mdo 16:6; 1 Kor 2:3]
14na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu.[#Mdo 14:11,12]
15Kuko wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi.
16Je! Nimekuwa adui yenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli?[#Amo 5:10]
17Hao wana shauku nanyi, lakini si kwa nia nzuri, bali wanataka kuwafungia nje, ili kwamba ninyi mwaonee wao shauku.[#Gal 1:7]
18Navyo ni vizuri kuonewa shauku katika neno jema sikuzote, wala si wakati nikiwapo mimi pamoja nanyi tu.
19Watoto wangu wadogo, ambao nawaonea uchungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;[#1 Kor 4:15]
20laiti ningekuwapo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu.
21Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria?[#Gal 3:23]
22Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Abrahamu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mwingine kwa mwanamke huru.[#Mwa 16:15; 21:2,9]
23Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwanamke huru kwa ahadi.[#Rum 9:7-9; Mwa 17:16]
24Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri.[#Gal 5:1; Rum 8:15]
25Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa yuko utumwani pamoja na watoto wake.
26Bali Yerusalemu wa juu ni muungwana, naye ndiye mama yetu sisi.[#Ebr 12:22]
27Kwa maana imeandikwa,[#Isa 54:1]
Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa;
Paza sauti, ulie, wewe usiye na uchungu;
Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi
Kuliko wa huyo aliye na mume.
28Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi.
29Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.[#Mwa 21:9]
30Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa muungwana.[#Mwa 21:10,12; Yn 8:35]
31Kwa hiyo, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye muungwana.[#Gal 3:29]