The chat will start when you send the first message.
1Upendano wa ndugu na udumu.[#Yn 13:34; 2 Pet 1:7]
2Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.[#Mwa 18:1-8; 19:1-3; Rum 12:13; 1 Pet 4:9]
3Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili.[#Mt 25:36]
4Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.[#Gal 5:19,21; Efe 5:5]
5Msiwe na tabia ya kupenda fedha; muwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kamwe, wala sitakuacha.[#Kum 31:6,8; Yos 1:5; 1 Tim 6:6]
6Hata tunathubutu kusema,[#Zab 118:6]
Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa;
Mwanadamu atanitenda nini?
7Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.[#1 Kor 4:16]
8Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.[#1 Kor 3:11; Ufu 1:17]
9Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.[#Efe 4:14; Rum 14:17; 2 Kor 1:21]
10Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiayo ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake.[#Ebr 8:4,5]
11Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi.[#Law 16:27]
12Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.[#Mt 21:39; Yn 9:22]
13Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutuma yake.[#Ebr 11:26; 12:2]
14Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.[#Ebr 11:10; 12:22]
15Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamalo jina lake.[#Law 7:12; 2 Nya 29:31; Zab 50:14,23; Isa 57:19; Hos 14:2]
16Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.[#Flp 4:18]
17Watiini viongozi wenu, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa huzuni; maana haitawafaa ninyi.[#1 The 5:12; Eze 3:17]
18Tuombeeni; maana tunaamini kwamba tuna dhamiri njema, tukitaka kuwa na mwenendo mwema katika mambo yote.[#2 Kor 1:12; Mdo 24:16]
19Nami nawasihi zaidi sana kufanya hayo ili nirudishwe kwenu upesi.
20Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu,[#Isa 63:11; 55:3; Zek 9:11; Yer 32:40; Eze 37:26; Yn 10:12; 1 Pet 2:25]
21awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.
22Lakini nawasihi, ndugu, mchukuliane na neno hili lenye maonyo maana nimewaandikia kwa maneno machache.[#Yak 1:21]
23Jueni ya kuwa ndugu yetu Timotheo amekwisha kufunguliwa; ambaye, akija upesi, nitaonana nanyi pamoja naye.
24Wasalimuni viongozi wenu wote, na watakatifu wote; hao walio wa Italia wanawasalimu.
25Neema na iwe nanyi nyote.