Waraka kwa Waebrania 4

Waraka kwa Waebrania 4

Pumziko aliloahidi Mungu

1Basi, ikiwa ingalipo ahadi ya kuingia katika pumziko lake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa.[#Zab 95:11]

2Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa Habari Njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia.

3Maana sisi tulioamini tunaingia katika pumziko lile; kama vile alivyosema,[#Zab 95:11]

Kama nilivyoapa kwa hasira yangu,

Hawataingia pumzikoni mwangu:

ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.

4Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote;[#Mwa 2:2]

5na tena kunena hapa napo, Hawataingia pumzikoni mwangu.[#Zab 95:11]

6Basi, kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao,

7aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo, kama ilivyonenwa tangu zamani,[#Zab 95:7-8]

Leo, kama mkisikia sauti yake,

Msifanye mioyo yenu migumu.

8Maana kama Yoshua angaliwapa pumziko, asingaliinena siku nyingine baadaye.[#Kum 31:7; Yos 22:4]

9Basi, limesalia pumziko la sabato kwa watu wa Mungu.

10Kwa maana yeye aliyeingia katika pumziko lake amepumzika mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyopumzika katika kazi zake.[#Mwa 2:2; Ufu 14:13]

11Basi, na tufanye bidii kuingia katika pumziko lile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.

12Maana neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena ni jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.[#Yer 23:29; Isa 49:2; Efe 6:17; Yn 12:48; Ufu 19:15]

13Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, maana vitu vyote ni tupu na kuwekwa wazi machoni pake yeye ambaye tunapaswa kuwajibika kwake.

Yesu aliye Kuhani Mkuu

14Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu.[#Ebr 3:1; 6:20; 7:26; 8:1; 9:11]

15Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa kama sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.[#Ebr 2:17]

16Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.[#1 Yoh 3:21; Rum 3:25]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya