The chat will start when you send the first message.
1Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi makabila ya watu mlio mbali sana; BWANA ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu.[#Mt 1:20; Lk 1:15; Yer 1:5]
2Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha;[#Hos 6:5; Ebr 4:12; Ufu 1:16]
3akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.[#Zek 3:8; Mt 17:17; Yn 13:31]
4Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina BWANA, na thawabu yangu ina Mungu wangu.[#Eze 3:19]
5Na sasa BWANA asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya BWANA, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu);
6naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuyainua makabila ya Yakobo, na kuwarejesha watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.[#Isa 9:2; 42:6; Lk 2:32; Mdo 13:47; 26:23]
7BWANA, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya BWANA aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua.
8BWANA asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa;[#Zab 69:13; 2 Kor 6:2]
9kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho.[#Isa 42:7; Zek 9:12]
10Hawataona njaa, wala hawataona kiu; joto halitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.[#Zab 22:26; 121:6; 23:2; Yn 6:35; Ufu 7:16-17]
11Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia zangu zote kuu zitainuliwa.
12Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu.
13Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi;
Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima;
Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake,
Naye atawahurumia watu wake walioteswa.
14Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.
15Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.[#Zab 103:13; Mt 7:11; Rum 11:29]
16Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.[#Kut 13:9; Wim 8:6; Zek 2:8]
17Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako.
18Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema BWANA, hakika utajivika hao wote kama pambo, nawe utajipamba kwao kama bibi arusi.[#Mit 17:6]
19Maana kuhusu mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali.[#Isa 54:1,2; Zek 2:4]
20Watoto ulionyang'anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa.[#Mt 3:9; Rum 11:11]
21Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami niko peke yangu, nimehamishwa, ninatangatanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, niliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi?[#Mwa 42:13; Yer 31:15]
22Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwainulia makabila ya watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao.
23Na wafalme watakuwa baba zako walezi, na malkia zao mama zako walezi; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni BWANA, tena waningojeao hawatatahayarika.[#Zab 72:9; 34:22; Mik 7:17; Rum 5:5]
24Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka wake, au mateka wa mtu katili kuokoka?[#Mt 12:29; Lk 11:21]
25Naam, BWANA asema hivi, Hata mateka wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka wake aliye katili wataokoka; kwa maana nitapambana na yeye abishanaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu.
26Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na watu wote watajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.[#Ufu 14:20; Zab 9:16; Isa 43:3]