The chat will start when you send the first message.
1Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Yudea, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitaka kumwua.[#Mk 9:30; Lk 9:51]
2Na sikukuu ya Wayahudi, sikukuu ya vibanda, ilikuwa karibu.[#Law 23:34; Kum 16:13]
3Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Yudea, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya.[#Yn 2:12; Mt 12:46; Mdo 1:14]
4Kwa maana hakuna mtu afanyaye mambo kwa siri, naye yeye mwenyewe anataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu.
5Maana hata nduguze hawakumwamini.[#Mt 13:55]
6Basi Yesu akawaambia, Wakati wangu haujafika bado; ila wakati wenu sikuzote upo.[#Yn 2:4]
7Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu.[#Yn 15:18]
8Pandeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sipandi bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa wakati wangu haujatimia.
9Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alibaki huko Galilaya.
10Hata ndugu zake walipokwisha kupanda kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipopanda, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.
11Basi Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule?
12Kukawa na manung'uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema. Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano.
13Lakini hakuna mtu aliyemsema waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.[#Yn 9:22; 12:42; 19:38]
14Hata ikawa katikati ya sikukuu Yesu alipanda kuingia hekaluni, akafundisha.
15Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma?[#Mt 13:54; Lk 2:47]
16Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenituma.[#Yn 12:49]
17Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu.
18Yeye anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali yeye anayetafuta utukufu wake aliyemtuma, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu.[#Yn 5:41,44]
19Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati. Mbona mnatafuta kuniua?[#Yn 5:16,18,47; Mdo 7:53; Rum 2:17-29]
20Mkutano wakajibu, Ama! Una pepo! Ni nani anayetafuta kukuua?[#Mk 3:21; Yn 8:48,52; 10:20]
21Yesu akajibu, akawaambia, Mimi nilitenda kazi moja, nanyi nyote mnaistaajabia.[#Yn 5:16]
22Musa aliwapa tohara; lakini si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwa mababa; nanyi mwatahiri mtu siku ya sabato.[#Mwa 17:10; Law 12:3]
23Basi ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili Torati ya Musa isije ikavunjika, mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nilimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya sabato?[#Yn 5:9]
24Basi msihukumu kwa kuangalia kwa nje tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki.[#Yn 8:15; #7:24 Katika Kigiriki ni ‘hukumu ya macho’.]
25Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue?[#Yn 7:19]
26Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Inawezekana hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo?
27Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako.[#Yn 7:41]
28Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenituma ni wa kweli, msiyemjua ninyi.
29Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.[#Mt 11:27]
30Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.[#Yn 8:20; 13:1; Lk 22:53]
31Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu?[#Yn 8:30; 10:42; 11:45; 12:42]
32Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung'unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate.
33Basi Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake yeye aliyenituma.[#Yn 13:33]
34Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja.[#Yn 8:21; 13:36; 17:24]
35Basi Wayahudi wakasemezana, Huyu atakwenda wapi hata sisi tusimwone? Ati! Atakwenda kwa Utawanyiko wa Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki?
36Ni neno gani hilo alilolisema, Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja?
37Katika siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.[#Law 23:36; Yn 4:10,14]
38Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.[#Eze 47:1,12; Zek 13:1; 14:8; Yoe 2:28; 3:18; Isa 44:3; 55:1; 58:11]
39Na neno hilo alilisema kuhusu Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.[#Yn 16:7; 2 Kor 3:17]
40Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule.[#Yn 6:14; Kum 18:15]
41Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya?[#Yn 1:46]
42Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi?[#2 Sam 7:12; Mik 5:2; Mt 2:5,6; 22:42; Zab 89:3]
43Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake.[#Yn 9:16]
44Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika.[#Yn 7:30]
45Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta?[#Yn 7:32]
46Wale watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu yeyote kama huyu anavyonena.[#Mt 7:28,29]
47Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika?
48Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?[#Yn 12:42]
49Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa.
50Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao),[#Yn 3:1-2]
51Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?[#Kum 1:16,17; 19:15]
52Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Chunguza, na utaona kuwa Galilaya hakutatoka nabii.[#Yn 1:46; 7:41]