The chat will start when you send the first message.
1Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya Waisraeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia.
2BWANA akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake.[#Yos 2:9; Amu 11:21; 2 Sam 5:19; Neh 9:24; Dan 5:18,19]
3Nanyi mtauzunguka mji huu, wapiganaji wote, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita.
4Na makuhani saba watachukua baragumu saba za pembe za kondoo dume, watatangulia mbele za hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga baragumu zao.[#Amu 7:16; Hes 10:8]
5Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo dume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia kwa mlio wa baragumu, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili.
6Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la Agano, tena makuhani saba na wachukue mabaragumu saba za pembe za kondoo dume watangulie mbele ya sanduku la BWANA.
7Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la BWANA.
8Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua baragumu saba za pembe za kondoo dume mbele za BWANA, watatangulia, wakayapiga hayo mabaragumu; nalo sanduku la Agano la BWANA likawafuata.[#Yos 4:13]
9Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani walioyapiga mabaragumu, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakiyapiga mabaragumu walipokuwa wakienda.[#Hes 10:25; Isa 42:12,13]
10Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lolote lisitoke kinywani mwenu, hadi siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele.
11Basi akalipeleka sanduku la BWANA liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa humo kambini.
12Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la BWANA.[#Kum 31:25]
13Na wale makuhani saba wakayachukua mabaragumu saba ya pembe za kondoo dume mbele ya sanduku la BWANA, wakaenda huku wakiyapiga mabaragumu; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la BWANA; huku makuhani wakiyapiga mabaragumu bila kukoma.[#1 Nya 15:26; Gal 6:9]
14Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita.
15Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ni siku hiyo tu ambapo waliuzunguka huo mji mara saba.
16Hata mara ya saba makuhani wakayapiga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu.[#Amu 7:20; 2 Nya 13:14]
17Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma.[#Mwa 12:3; Yos 2:4; 1 Sam 15:6; Mt 10:41; 25:40; Ebr 6:10; 11:31; Yak 2:25]
18Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtaifanya kambi ya Israeli kuwa imelaaniwa na kuifadhaisha.[#Kum 7:26; 13:17; Yos 7:1,11,12; Isa 52:11; Rum 12:9; 2 Kor 6:17; Efe 5:11; 1 The 5:22; Yos 7:25; 1 Fal 18:17,18; Yon 1:12]
19Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA.
20Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia mlio wa mabaragumu hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka chini kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akisonga mbele kukabili; wakautwaa huo mji.[#Ebr 11:30]
21Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume, wanawake, watoto na wazee, na ng'ombe, kondoo na punda, kwa upanga.[#Kum 7:2; 20:16,17; 1 Sam 15:3,8,18,19; 1 Fal 20:42; Yer 48:18; Ufu 18:21]
22Naye Yoshua akawaambia wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba, mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia.[#Yos 2:14; Ebr 11:31]
23Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya kambi ya Israeli.[#Yos 2:13]
24Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya BWANA.
25Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko.[#Ebr 11:31; Mt 1:5]
26Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe na BWANA mtu yule atakayeinuka na kutaka kuujenga tena mji huu wa Yeriko; atakayeweka msingi wake mzaliwa wake wa kwanza na afe. Tena atakayesimamisha malango yake mtoto wake wa kiume aliye mdogo na afe.[#1 Fal 16:34; Mal 1:4]
27Basi BWANA alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote.[#Mwa 39:2; Kum 31:8,23; Yos 1:5; 3:7; Amu 1:19; 2 Sam 7:9; 8:6; Rum 8:31; Yos 9:1,3; 1 Sam 2:30]