The chat will start when you send the first message.
1Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata.[#Mk 1:40-44; Lk 5:12-14]
2Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.
3Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika.
4Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila nenda zako, ukajioneshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao.[#Law 13:49; 14:1-32; Mt 9:30; Mk 7:36; Lk 17:14]
5Na alipoingia Kapernaumu, afisa mmoja alimjia,[#Lk 7:1-10; #Yn 4:47]
6akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana.
7Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye.
8Yule afisa akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona.
9Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.
10Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli.[#Mt 15:28]
11Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;[#Lk 13:29; Isa 49:12; 59:19; Mal 1:11; Zab 107:3]
12bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.[#Mt 22:13; 24:51; 25:30; Lk 13:28]
13Naye Yesu akamwambia yule afisa, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona wakati ule ule.[#Mt 9:29; 15:28]
14Na Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani akiugua homa.[#Mk 1:29-34; Lk 4:38-41; #1 Kor 9:5]
15Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia.
16Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa wagonjwa,
17ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,[#Isa 53:4]
Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu,
Na kuyachukua magonjwa yetu.
18Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng'ambo.[#Mk 4:35; Lk 8:22]
19Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako.[#Lk 9:57-60]
20Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.[#2 Kor 8:9]
21Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu.[#1 Fal 19:20]
22Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.[#Yn 1:43; 5:25; Rum 6:13]
23Akapanda katika mashua, wanafunzi wake wakamfuata.[#Mk 4:36-41; Lk 8:23-25; #Zab 4:8]
24Kukawa na msukosuko mkuu baharini, hata mashua ikafunikwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi.
25Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia.
26Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu.[#Mt 14:31; 16:8]
27Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?
28Naye alipofika ng'ambo, katika nchi ya Wagadara, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wakitoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile.[#Mk 5:1-17; Lk 8:26-37]
29Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya wakati wetu?[#Lk 4:41; 2 Pet 2:4]
30Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakila.
31Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe.
32Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakateremka kwa kasi gengeni hadi baharini, wakafa maji.
33Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote na habari za wale wenye pepo pia.
34Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke katika nchi yao.