The chat will start when you send the first message.
1Haleluya.
Msifuni BWANA kutoka mbinguni;
Msifuni katika mahali palipo juu.
2Msifuni, enyi malaika wake wote;[#Dan 7:10; Ebr 1:7]
Msifuni, majeshi yake yote.
3Msifuni, jua na mwezi;
Msifuni, nyota zote zenye mwanga.
4Msifuni, enyi mbingu za mbingu,[#1 Fal 8:27]
Nanyi maji mlioko juu ya mbingu.
5Na vilisifu jina la BWANA,[#Ebr 11:3]
Kwa maana aliamuru, vikaumbwa.
6Amevithibitisha hata milele na milele,[#Yer 33:25]
Ametoa amri wala haitapita.
7Msifuni BWANA kutoka nchi,[#Isa 43:20]
Enyi nyangumi na vilindi vyote.
8Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke,
Upepo wa dhoruba utimizao neno lake.
9Milima na vilima vyote,[#Isa 49:13]
Miti yenye matunda na mierezi yote.
10Hayawani, na wanyama wafugwao,
Vitambaavyo, na ndege wenye mbawa.
11Wafalme wa dunia, na watu wote,[#Mdo 17:28]
Wakuu, na watawala wote wa dunia.
12Vijana wa kiume, na wanawali,
Wazee, na watoto;
13Na walisifu jina la BWANA,[#Isa 6:3; Flp 2:9]
Maana jina lake peke yake limetukuka;
Adhama yake i juu ya nchi na mbingu.
14Naye amewainulia watu wake pembe,[#Efe 2:17; 1 Pet 2:9]
Sifa za watauwa wake wote;
Wana wa Israeli, watu walio karibu naye.
Haleluya.