The chat will start when you send the first message.
1Ee BWANA, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.
2Hukumu yangu na itoke kwako,
Macho yako na yatazame mambo ya adili.
3Umenijaribu moyo wangu, umenijia usiku,[#Ayu 23:10; Yak 3:2]
Umenichunguza usione neno;
Nimenuia kinywa changu kisikose,
4Kuhusu matendo ya wanadamu;[#Rum 12:2]
Kwa neno la midomo yako
Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.
5Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako,
Hatua zangu hazikuondoshwa.
6Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
7Dhihirisha fadhili zako za ajabu
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kulia
Uwaokoe kutoka kwa adui zao.
8Unilinde kama mboni ya jicho,[#Kum 32:10]
Unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako;
9Wasinione wasio haki wanaonionea,
Adui za roho yangu wanaonizunguka.
10Wamejawa na ukaidi,
Kwa vinywa vyao wanajigamba.
11Wamenifuatia; na sasa wananizunguka,[#1 Sam 23:26]
Na kuyakaza macho yao watuangushe chini.
12Kama mfano wa simba atakaye kurarua,
Kama mwanasimba aoteaye katika maotea yake.
13Inuka, Ee BWANA, umkabili, umwangushe,
Kwa upanga wako uniokoe nafsi yangu na mtu mbaya.
14Ee BWANA, kwa mkono wako uniokoe na watu,
Watu wa dunia hii ambao fungu lao liko katika maisha haya.
Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako,
Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao,
15Bali mimi nikutazame uso wako katika haki,[#Ayu 19:26,27; Kol 1:15]
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.