Zaburi 22

Zaburi 22

Ombi la ukombozi katika shida na ukatili

1Mungu wangu, Mungu wangu,[#Mt 27:46; Mk 15:34; Ebr 5:7]

Mbona umeniacha?

Mbona U mbali na wokovu wangu,

Na maneno ya kuugua kwangu?

2Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu

Na wakati wa usiku lakini sipati raha.

3Lakini Wewe U Mtakatifu,[#Isa 6:3; Ufu 4:8]

Utukuzwaye na sifa za Israeli.

4Baba zetu walikutumainia Wewe,

Walitumainia, na Wewe ukawaokoa.

5Walikulilia Wewe wakaokoka,

Walikutumainia, nao hawakuaibika.

6Lakini mimi ni mdudu wala si mtu,[#Isa 53:3]

Nimedharauliwa na kupuuzwa na watu.

7Wote wanionao hunicheka sana,[#Mt 27:39; 9:24; Mk 15:20,29; Lk 23:35; 16:14]

Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;

8Husema, Umtegemee BWANA; na amponye;[#Mt 27:43]

Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.

9Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni,

Ulinisalimisha matitini mwa mama yangu.

10Kwako nilitupwa tangu tumboni,

Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.

11Usiwe mbali nami maana taabu i karibu,

Kwa maana hakuna msaidizi.

12Mafahali wengi wamenizunguka,

Walio hodari wa Bashani wamenisonga;

13Wananifumbulia vinywa vyao,[#Zab 35:21; 1 Pet 5:8]

Kama simba apapuraye na kunguruma.

14Nimemwagika kama maji,

Mifupa yangu yote imeteguka,

Moyo wangu umekuwa kama nta,

Na kuyeyuka ndani ya moyo wangu.

15Nguvu zangu zimekauka kama gae,[#Mit 17:22]

Ulimi wangu waambatana na taya zangu;

Unaniweka katika mavumbi ya mauti

16Kwa maana mbwa wamenizunguka;[#Zek 12:10; Lk 23:33; Yn 20:27]

Kusanyiko la waovu wamenisonga;

Wamenidunga mikono na miguu.

17Naweza kuihesabu mifupa yangu yote;

Wao wananitazama na kunikodolea macho.

18Wanagawanya nguo zangu,[#Mt 27:35; Mk 15:24; Lk 23:34; Yn 19:24]

Na vazi langu wanalipigia kura.

19Nawe, BWANA, usiwe mbali,

Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.

20Uniponye nafsi yangu na upanga,

Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.

21Kinywani mwa simba uniokoe;[#2 Tim 4:17]

Naam, toka pembe za nyati umenijibu.

22Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,[#Ebr 2:12; Yn 20:17]

Katikati ya kusanyiko nitakusifu.

23Ninyi mnaomcha BWANA, msifuni,

Enyi nyote mlio wazawa wa Yakobo, mtukuzeni,

Mcheni, enyi nyote mlio wazawa wa Israeli.

24Maana hapuuzi

Wala kuchukizwa na mateso ya anayeteswa,

Wala hamfichi uso wake,

Bali humsikia akimlilia.

25Kwako zinatoka sifa zangu

Katika kusanyiko kubwa.

Nitaziondoa nadhiri zangu

Mbele yao wamchao.

26Wapole watakula na kushiba,[#Yn 6:51,57]

Wamtafutao BWANA watamsifu;

Mioyo yenu na iishi milele.

27Miisho yote ya dunia itakumbuka,[#Zab 2:8]

Na watu watamrejea BWANA;

Jamaa zote za mataifa watamsujudia.

28Maana ufalme ni wa BWANA,[#Zab 47:7-9; Zek 14:9; Mt 6:13]

Naye ndiye awatawalaye mataifa.

29Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,[#Isa 26:19]

Humwinamia wote washukao mavumbini;

Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,

30Wazawa wake watamtumikia.

Zitasimuliwa habari za BWANA,

Kwa kizazi kitakachokuja,

31Watautangaza wokovu wake kwa watakaozaliwa,

Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya