Zaburi 32

Zaburi 32

Shangwe kwa kusamehewa

1Heri aliyesamehewa dhambi,[#Rum 4:7-8; Zab 85:2]

Na kuondolewa makosa yake.

2Heri ambaye BWANA hamhesabii hatia,[#Law 17:4; Rum 5:13; Yn 1:47; 2 Kor 1:12]

Na ambaye rohoni mwake hamna hila.

3Nilipokosa kuungama dhambi zangu, mifupa yangu ilipooza

Kwa kulia kwangu mchana kutwa.

4Kwa maana mchana na usiku

Mkono wako ulinilemea.

Jasho langu likakauka hata nikawa

Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.

5Ndipo nikakuungamia dhambi yangu,[#Mit 28:13; Isa 65:24; Lk 15:18]

Wala sikuuficha upotovu wangu.

Nilisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA,

Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.

6Kwa hiyo, hebu kila akuaminiye[#1 Tim 1:16; Isa 55:6; Yn 7:34]

Akuombe awapo katika dhiki.

Hakika maji makuu yafurikapo,

Hayatamfikia yeye.

7Kimbilio langu utanilinda nisipate mateso,[#Zab 9:9; Mit 18:10; Isa 4:6; Mt 23:37; Kol 3:3]

Utanizungusha nyimbo za kufurahia wokovu wangu.

8Nitakufundisha na kukuonesha njia utakayoiendea;[#Isa 48:17]

Nitakushauri, jicho langu likikutazama.

9Msiwe kama farasi wala nyumbu,

Wasiokuwa na akili.

Kwa matandiko ya lijamu na hatamu

Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia.

10Naye mtu mwovu ana mapigo mengi,[#Mit 13:21; Zab 34:8; Mit 16:20; Yer 17:7]

Bali amtumainiaye BWANA fadhili zitamzunguka.

11Mfurahieni BWANA;

Shangilieni, enyi wenye haki

Pigeni vigelegele vya furaha;

Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya